Morocco yatoa ndege kuokoa wanaouzwa Libya

MFALME wa Morocco, Mohammed VI amejitolea ndege kuokoa maelfu ya Waafrika waliokwama nchini Libya na kudaiwa kuuzwa kwa Dola za Marekani 400 hadi 800 kwa mnada kwenye soko la watumwa.

Tayari Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameelezea utayari wa kuchukua wahamiaji 30,000 wa Afrika waliokwama Libya baada ya kushindwa kwenda barani Ulaya, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais wa Guinea, Alpha Conde alisema jijini Abidjan, Ivory Coast kuwa, ndege hizo zinatarajiwa kuokoa Waafrika 3,800 kwa kushirikiana na kikosi kazi kinachoongozwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Inadaiwa kuna wahamiaji na wakimbizi kati ya 400,000 hadi 700,000 nchini Libya. Waafrika hao wapo vizuizini kwenye kambi zilizopo jirani na Tripoli na kwingineko. Wakati wa kufungwa kwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, alieleza kushtushwa na yanayoendelea Libya na kuagiza hatua zichukuliwe haraka.

Inadaiwa kuwa, wakiwa njiani kutoka kwenye nchi zao na hata wanapofika Libya Waafrika wanateswa, wanapigwa, wananyanyaswa, wanakufa kwa njaa au kuuawa. Inadaiwa kuwa, wanawake wanadhalilishwa kingono ikiwa ni pamoja na kulazimishwa kufanya ukahaba.

Guterres ameagiza mamlaka zichunguze haraka taarifa za kuteswa, kudhalilishwa, kuuzwa, na kuuawa kwa Waafrika nchini humo na pia wahusika wachukuliwe hatua. Baadhi ya wahamiaji na wakimbizi hao wanatoka kwenye nchi za Senegal, Cameroun, Nigeria, Ghana, Zambia, Gambia, Sudan, Chad na Niger.

Katika mkutano huo, Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk alisema, EU, AU, na UN hawatakuwa wamefanikiwa kama hawatahakikisha watu waliokwama Libya na kwingineko wanarudi kwao salama.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame alisema katika mkutano huo kuwa, shida na mateso wanayopata wahamiaji na wakimbizi Waafrika nchini Libya ni kipimo cha ubinadamu na ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya na lazima mabara hayo yashirikiane kumaliza tatizo hilo.

UN, AU na EU wamekubaliana kuwa na kikosi kazi kuokoa maelfu ya Waafrika waliokuwa wamekwama Libya baada ya mamlaka za nchi hiyo kuwazuia wasiende Ulaya. Makubaliano hayo ni matokeo ya mkutano jijini Abijan, uliohudhuriwa na Katibu Mkuu wa UN, Guterres, Mwenyekiti wa tume ya AU, Moussa Faki Mahamat, Rais wa tume ya Ulaya Jean-Claude Juncker, na Makamu wa Rais wa Baraza la Ulaya, Federica Mogherini.

Siku chache ziilizopita, kulikuwa na kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la UN kuhusu tatizo hilo. Maelfu ya Waafrika wanafika Libya kwa kusafirishwa na mitandao ya wahalifu yenye makazi nchini humo na katika nchi wanapotoka wakimbizi na wahamiaji hao.

Kwa mujibu wa Balozi Mdogo wa Libya nchini Tanzania, Saleh Kuza, kuna makundi ya wahalifu wanaofanya biashara kusafirisha watu hasa vijana kwa ahadi ya kuwapeleka Ulaya. Balozi Kuza amesema, kuna biashara ya kuuza binadamu nchini Libya lakini si kuwauza kama watumwa.

Amesema, hata video iliyooneshwa kwenye kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani si ya watu kuuzwa kama watumwa ila ni majibizano ya bei ya kuwasafirisha watu kuwapeleka Ulaya. Alisema, wengi wa wanaosafirishwa wanatoka kwenye nchi zenye changamoto za kiusalama au ukosefu mkubwa wa ajira.

Kwa mujibu wa Balozi huyo, hakuna Watanzania wanaokwenda Libya kwa lengo la kutorokea kwenda Ulaya. Taarifa zinadai kuwa, kila mtu anayesafirishwa kutoka alipo kwenda Libya anatakiwa kuwalipa wasafirishaji kati ya Dinari 1,000 za Libya (Dola za Marekani 735) hadi Dinari 1,500 (Dola za Marekani 1,100).

Hivi karibuni kituo cha televisheni cha CNN kilionesha wahamiaji na wakimbizi hao wakiuzwa kwa mnada kwenye soko la watumwa jirani na Tripoli. Katika mnada huo, wauzaji waliwanadi wanaume waliokuwa wakiuzwa kuwa wana nguvu na wangefaa kwa kazi ya kulima.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisema jijini Abidjan, kuwa, Libya imekubaliana na EU na viongozi wa Afrika kuruhusu wahamiaji walio kwenye vizuizi katika kambi mbali waondolewe.