Rwanda yatangaza mabadiliko makubwa zabuni za serikali

SERIKALI ya Rwanda imewasilisha bungeni muswada wa kubadili sheria ya zabuni ili bidhaa za nchini humo zipate upendeleo wa angalau asilimia 65 kwenye zabuni za serikali.

Mabadiliko hayo yana lengo la kuwezesha utekelezaji sera na kampeni ya kuhamasisha kuthamini bidhaa na huduma za nchini humo. Sheria ya sasa inatoa upendeleo wa asilimia 10 kwa bidhaa na huduma za ndani kwa zabuni zinazoshirikisha waombaji kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachama wa Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

Kwa mujibu wa Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Vincent Munyeshyaka, serikali inataka kubadili utaratibu ili bidhaa na huduma za nchini humo zipate upendeleo na kupunguza nguvu ya kampuni za nje kwenye zabuni za serikali.

Waziri Munyeshyaka alisema, wazalishaji binafsi wanaotengeneza bidhaa nchini humo watapewa fursa muhimu ya kushinda zabuni za serikali, na kwamba, mabadiliko hayo hayataathiri ubora wa bidhaa na huduma.

Aliyasema hayo wakati wa maonesho ya tatu ya bidhaa zinatengenezwa Rwanda kwenye viwanja vya maonesho vya Gikondo jijini Kigali. Maonesho hayo yaliyoanza Novemba 29 na kushirikisha wazalishaji 420 yanamalizika leo.

Muswada huo tayari umewasilishwa bungeni baada ya Baraza la Mawaziri kuupitisha. Kwa mujibu wa Waziri Munyeshyaka, Bunge linaupitia na likiupitisha itatangazwa gazetini.