Tanzania ya kwanza idadi ya watu EAC

WAKATI Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikijivunia kuwa na idadi ya watu takribani milioni 170, hivyo kufanya kuwa soko la uhakika kwa bidhaa za ndani, Tanzania ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi ya watu milioni 52.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile wakati wa uzinduzi wa taarifa ya hali ya idadi ya watu duniani ya mwaka 2017 iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).

Alisema kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa afya na idadi ya watu kwa mwaka 2015/16 kuna ongezeko kubwa la watu kwa milioni 2.7 na kwa sensa ya mwaka 2012 hadi sasa idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa kasi ambapo serikali inahitaji kujipanga kuzingatia ongezeko hilo.

Alisema vigezo vinavyotumika ni viwili ambvyo ni elimu na umasikini na kwamba vina mchango mkubwa katika kubadili hali ya afya ya wanawake hasa katika suala la uzazi, ambapo hali hiyo ikitatuliwa, itapunguza changamoto nyingi zinazoleta tofauti miongoni mwa jamii.

“Hatukatazi watu kuzaa, lakini ongezeko hilo ni kubwa sana, inapaswa liendane na rasilimali zilizopo,” alisema Dk Ndungulile na kuhamasiaha wanaume kuangalia uwezekano wa kupanga uzazi.

Idadi ya sasa ya Watanzania ni hadi kufikia mwaka huu, ingawa kwa mujibu wa takwimu za Sensa za Watu na Makazi za Mwaka 2012, Tanzania ilikuwa na watu 44,929,002. Tanzania sasa inafuatiwa na Kenya yenye watu milioni 49, Uganda yenye watu milioni 42 na kisha Sudan Kusini, Rwanda na Burundi ambazo kila moja ina wastani wa watu milioni 12.

Aidha, imeelezwa kutokana na ongezeko la kasi la watu, ifikapo mwaka 2050 Tanzania inakadiriwa itakuwa na watu milioni 100 na miaka 50 baadaye, yaani mwaka 2100 Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi 10 duniani zenye idadi kubwa ya watu.

Kwa wataalamu wa masuala ya maendeleo, idadi ya watu huchukuliwa kuwa ni mtaji katika ustawi wa shughuli za kiuchumi. Mbali ya ukubwa wa idadi ya watu, Tanzania pia inaongoza kwa ukubwa wa eneo, ikiwa na kilometa za mraba 947,303 (ni nchi ya 31 kwa ukubwa duniani).

Kwa EAC, inafuatiwa na Sudan Kusini yenye kilometa za mraba 619,745, Kenya yenye kilometa za maraba 580,367, Uganda yenye kilometa za mrava 241,038, Burundi 27,834 na Rwanda yenye ukubwa wa kilometa za mraba 26,338.