RC agharamia safari kuombea eneo lililokithiri kwa ajali Singida

MKUU wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi amesema ofisi yake imetoa shilingi laki tano kugharamia safari za viongozi wa madhehebu ya dini ili waende kufanya maombi maalumu kwenye maeneo yaliyokithiri kwa ajali za barabarani mkoani hapa.

Dk Nchimbi ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika kwenye Kituo cha Zamani cha Magari ya abiria mjini Singida.

Alisema kuwa anatambua kuwa karibu kila wilaya mkoani humo kuna eneo ambalo ajali hutokea mara kwa mara lakini bado haamini kuwa hayo ni mapenzi ya Mungu bali ni balaa ambayo inahitaji maombezi ili mkoa uweze kuondokana nayo.

"Karibu kila wilaya ina eneo ambalo ajali haziishi kutokea. Imani yangu Mungu hajanipa mkoa wenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya ajali. Nimekubaliana na viongozi wangu wa dini waende kwenye maeneo hayo na kuomba Mungu atuondolee balaa hiyo.

Ili kufanikisha suala hili, Ofisi yangu imetoa jumla ya Sh 500,000 kugharamia safari zao", alisema. Aidha, alitoa mwito kwa madereva wa vyombo vya moto kutii na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na sio kuendesha vyombo hivyo kwa kuogopa kamera za barabarani maarufu kama "tochi".

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa,Debora Magiligimba amewaagiza viongozi wa madereva wa bodaboda na bajaji kuhakikisha wanasimamia ipasavyo madereva wao ili kupunguza ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda huyo, jumla ya watu 68 walifariki kutokana na ajali za barabarani kati ya Januari na Oktoba mwaka huu ikilinganishwa na vifo 152 kwa kipindi kama hicho mwaka jana; hali inayoonesha kupungua kwa matukio hayo.