Wanafunzi 2,679 waliokata rufaa Bodi ya Mikopo waula

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha yenye wanafunzi 2,679 ambao wamepata mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya Sh bilioni 9.6 baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa rufaa zilizowasilishwa na wanafunzi hao.

Kati ya wanafunzi hao, 1,847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya Sh bilioni 6.84 na wengine 832 ni wale wanaoendelea na masomo lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita.

Wanafunzi hao wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 2.76. Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru (pichani) alisema Dar es Salaam jana kuwa orodha kamili ya wanafunzi waliofanikiwa kupata mikopo kupitia dirisha la rufaa pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo wanafunzi hao hivi sasa.

Badru alisema hatua hiyo inafanya jumla ya wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 108 kwa mwaka wa masomo 2017/2018 hadi sasa.

Alisema bajeti ya jumla kwa wanafunzi wote kwa mwaka 2017/18 ni Sh bilioni 427.54. Dirisha la rufaa lilifunguli wa kwa siku saba kuanzia Novemba 13, mwaka huu hadi Novemba 19, mwaka huu ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawakuwa wameridhika na upangaji wa mikopo na kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.

Wanafunzi waliohamishiwa mikopo yao Wakati huo huo, Bodi hiyo ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeanza kuhamisha mikopo iliyokuwa imeelekezwa katika vyuo tofauti na waliko kwa sasa.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Badru alisema jana kuwa mikopo ya wanafunzi 590 wa mwaka wa kwanza yenye thamani ya Sh bilioni 1.78 ambayo awali ilikuwa imepelekwa katika vyuo tofauti na walipo wanafunzi imehamishwa.

Alisema wanafunzi hao waliohamishiwa mikopo yao ni wale ambao walipangiwa mikopo na kupelekewa fedha zao katika vyuo ambavyo walipata udahili awali, ila baadaye wakaamua kujiunga na vyuo vingine ambavyo nako walipata udahili.

Alisema orodha kamili ya wanafunzi pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo hivi sasa. “Bodi ya Mikopo inaendelea kupokea orodha za wanafunzi waliosajiliwa katika vyuo mbalimbali na wale wenye mikopo, fedha zao zitahamishiwa katika vyuo walipo katika awamu zijazo,” alisema Badru.

Kuhusu mikopo kwa wahadhiri wa vyuo vikuu, Badru alisema jumla ya wanafunzi 45 wa Shahada za Uzamili na Uzamivu ambao ni wanataaluma na waajiriwa wa vyuo mbalimbali nchini wamepata mikopo yenye thamani ya Sh milioni 441.4 katika mwaka wa masomo wa 2017/2018.

Mikopo hiyo hutolewa na Bodi ya Mikopo kwa wanataaluma hao ili kuvijengea vyuo uwezo wa kitaaluma chini ya makubaliano kati ya Bodi ya Mikopo na vyuo hivyo.