Polisi Dar yaua watatu kwa ujambazi

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewaua watu watatu wanaodaiwa kuwa ni majambazi akiwemo raia wa Burundi.

Imeelezwa kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakijihusisha na matukio ya uporaji na mauaji katika maeneo mbalimbali ya jiji. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa alisema tukio hilo lilitokea Novemba 28 na 30, mwaka huu baada ya askari kufanya operesheni maalumu.

Alisema raia huyo wa Burundi aliyefahamika kwa jina la Fanuel Kamana ndio aliyekuwa mratibu wa matukio yote na akifanya tukio alikuwa anaigawaanaoshirikiana nao kipande kimoja kimoja ili isitumike wakati yeye akiwa Burundi.

Alisema awali baada ya kukamatwa na kufanya mahojiano nao watuhumiwa hao walikubali kuonesha silaha moja aina ya AK.47, magazini mbili na risasi 57 ambazo walikuwa wamezificha kwenye kichaka karibu na eneo la Ubungo Mawasiliano. Pia walionesha pikipiki mbili aina ya Boxer zenye namba za usajili MC 757 BCT rangi nyekundu na MC 946 BSE rangi nyeusi ambazo walizipora katika matukio mbalimbali.

Aliongeza kuwa walipohojiwa zaidi walisema wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha kwenye kichaka eneo la Ununio na wako tayari kwenda kuonesha silaha hizo. Alisema walipofika huko wakati wakishuka kwenye gari, Kamana alimvamia askari kwa lengo la kumpora silaha huku wenzake wawili wakijaribu kutoroka na ndipo walilpopigwa risasi na kujeruhiwa.

“Naomba niwaonye Watanzania ambao wamekuwa wakiwahifadhi wageni kuja kufanya matukio ya kihalifu waache mara moja kwani jeshi limejipanga kutokomeza matukio yote ya uhalifu kwa hiyo niwaambie hatutamuacha yeyote atakayeshirikiana na wahalifu,” alisema Mambosasa.

Mambosasa alisema majambazi hao waliwahishwa katika Hospitali ya Mwananyamala ili kupatiwa matibabu lakini madaktari walibaini kuwa tayari walishafariki dunia na miili hiyo imehifadhiwa hospitalini hapo kwa hatua za uchunguzi wa kitaalamu.

Aidha alisema majambazi hao walikiri kufanya matukio kadhaa ya uporaji na mauaji likiwemo tukio la mauaji lililotokea Kunduchi Mtongani Novemba 19, mwaka huu ambapo waliwaua madereva bodaboda na kupora pikipiki zao na kuziuza kwa Sh 800, 000.