Mwanafunzi mbaroni akiwa na sare za JWTZ

JESHI la Polisi, Kanda Maalumu Dar es Salaam linamshikilia Said Selemani (17), mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari ya Fahari iliyopo Goba, kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kujifanya ni mwanajeshi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa alisema mwanafunzi huyo alikamatwa eneo la Mbezi benki ya CRDB akiwa amevaa sare hizo za JWTZ huku akivuta sigara hadharani na kufanya vitendo vingine ambavyo haviendani na maadili ya askari aliyevaa sare.

Alisema mwanafunzi huyo alikuwa akilazimisha kupatiwa huduma kwa madai ya kuwa yeye ni mwanajeshi na alikuwa akipanda katika vyombo vya usafiri na kugoma kutoa nauli. Aliongeza kuwa katika mahojiano ya awali kijana huyo alijitambulisha ni askari kutoka kikosi cha 501 KJ kilichopo Lugalo, baada ya kubanwa zaidi alikiri kupata sare hizo kutoka kwa rafiki zake.