4 kizimbani kwa madai ya kubaka

WASHITAKIWA watatu, wakazi wa Mbezi Africana na mtoto mmoja, mkazi wa Ubungo Kibangu wamepandishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa tuhuma za kubaka.

Wakisomewa mashitaka hayo mbele ya hakimu Hanifa Mwingira, Mwendesha Mashitaka, Credo Rugaju alidai kwamba watuhumiwa watatu Richard Camali (27) na Elia Japhat (33) ambao ni mafundi ujenzi pamoja na Juma Ramadhani walitenda kosa hilo kwa pamoja.

Rugaju alidai kwamba watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 13, 2017 maeneo ya Mbezi Africana wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Watuhumiwa wote walikana shitaka na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo walihitajika kuwa na wadhamini wawili wakusaini ahadi ya dhamana ya laki tano.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Desemba 18 mwaka huu mahakamani hapo. Mashitaka mengine, yalimhusisha mtoto wa miaka kumi na saba (jina tunalihifadhi) ambaye ni fundi wa kushona nguo aliyepandishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka 10.

Akisomewa mashitaka hayo mbele ya hakimu Mwingira, msoma mashitaka Rugaju alidai kwamba mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Septemba 9, mwaka huu maeneo ya Ubungo Kibangu.

Mshitakiwa alikana shitaka hilo na kuachiwa kwa dhamana, ambapo kesi hiyo itatajwa tena Desemba 12, mwaka huu ambapo hakimu ametaka upande wa mlalamikaji kuhamishia kesi hiyo katika mahakama ya watoto Kisutu.