Mfumo wa kodi kufumuliwa

SERIKALI imesema iko tayari kupokea mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kodi na usimamizi wake katika taifa ili kuchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alisema hayo jana mjini hapa kwenye mkutano wa kujadili mchango wa sekta binafsi kwenye sera ya bajeti ya mwaka 2018/2019. Alisema serikali iko tayari kupokea mapendekezo kwenye kodi na usimamizi kwa lengo la kuboresha mfumo wa kodi katika nchi, uweze kutoa mchango unaotakiwa kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha katika mkutano huo alisihi wadau kupokea mapendekezo ya mfumo wa kodi ambao utaongeza nguvu kwa sekta binafsi.Msingi wa bajeti Akizungumza alisema kwamba kutokana na mazingira halisi yalivyo sasa, wadau wanastahili kuangalia kwa makini, mapendekezo na kuyajadili ili kuwa msingi wa bajeti ijayo kutokana na wahisani kupunguza mchango wao katika bajeti.

“Mkutano huu ni msingi wa kuandaa bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019, mkutano uzingatie azma ya serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda tunataka taifa liende mbele na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa ujumla,” alisema. Aidha alisema katika mkutano uliofanyika Oktoba mwaka huu baadhi ya masuala ya kodi yaliwasilishwa na kujadiliwa na yapo ambayo yamefanyiwa kazi.

Akizungumza mchango wa wahisani katika bajeti alisema kumekuwa na kushuka kwa misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo kutoka Sh trilioni 1.5 mwaka 2013/2014 hadi kufikia Sh bilioni 495. Pia alisema hata mikopo ya masharti nafuu imeshuka kutoka Sh trilioni 1.258 mwaka 2013/2014 na kufikia Sh trilioni 1.231 mwaka 2015/2016.

“Zamani tulikuwa tukipata misaada na mikopo sasa inapungua, wananchi wetu hawapati mahitaji ya msingi,” alisema na kuongeza kuwa mfumo mzuri wa kodi utawezesha serikali kujenga uwezo wa kutoa huduma zake kwa wananchi. Huduma za jamii Kuhusu huduma za jamii, Waziri Mpango alisema uzalishaji wa maji katika miji mikuu ya wilaya ni asilimia 36 tu ya mahitaji.

Alisema hata katika vifo vinavyotokana na uzazi sasa ni 556 katika kila vizazi hai 100,000 na lengo ni kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2020 vifo hivyo vipungue na kufikia 265 kwa kila vizazi hai 100,000. Aidha alisema dawa za magonjwa kama malaria, Ukimwi, kifua kikuu sehemu kubwa zimekuwa zikitegemea wafadhili, hali ambayo katika siku za usoni lazima idhibitiwe kwa kuwa wahisani wanaweza kuchoka.

Waziri Mpango alisema kwa upande wa vituo vya afya vilivyopo ni 507 kati ya 4,420 vinavyohitajika ikiwa ni sawa na asilimia 11.5, zahanati zipo 4,470 kati ya 12,545 zinazohitajika sawa na asilimia 35.6 ya mahitaji. Alisema katika elimu ya msingi kuna upungufu wa vyumba 182,899 vilivyopo 66,794 kwa upande wa sekondari vilivyopo ni 120,766 vinavyohitajika ni 266,872.

Alisema madarasa sekondari 39,620 kati ya madarasa 52,188 yanayohitajika huku matundu ya vyoo yaliyopo 167,466 kati ya 517,606 yanayohitajika kwa shule za msingi na sekondari yapo 66,604 kati ya 90,425 yanayohitajika. Alisema kimsingi pamoja na serikali kuwa na kazi kubwa ya kufanikisha huduma hizo bado kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari ni hafifu huku kukiwa na ufujaji wa mapato ya serikali.

Hoja ya serikali Katika hotuba yake Waziri Mpango alisema hata uwezo wa kutumia ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP) hapa nchini bado ni mdogo na kutaka juhudi kuongezwa ili serikali iweze kuwa na nguvu kubwa ya utendaji kwa kuwepo rasilimali fedha za kutosha.

“Mtoe mapendekezo ya mfumo wa kodi ambao utaongeza nguvu katika sekta binafsi,” alisema na kuongeza kuwa ni katika mfumo bora wa kodi utakaowezesha kuwapo na mchango mkubwa wa hiari wa kodi kutoka kwa wananchi na wadau wengine katika sekta binafsi.

Kauli ya TPSF Samwel Nyantahe ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Sekta Binafsi, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi alisema serikali ya awamu ya tano imewezesha sekta binafsi kushiriki uchumi wa nchi na kuuboresha ushirikiano kati kati ya serikali na sekta binafsi.

Alisema ili serikali kuwa na uwezo mkubwa ni vyema serikali kuwezesha wananchi. “TPSF wafanye kazi na serikali ili kuwezesha wananchi katika nyanja tofauti,” alisema Akichangia kwenye mkutano huo Luis Acaro kutoka TPSF alisema mkutano huo utawezesha sekta binafsi kutoa mawazo yao kwa serikali kwani wana mambo mengi lakini watakayozungumza ni masuala mtambuka yanayohusiana na kodi.

“Sekta binafsi lazima izungumze mambo yanayowakabili ili serikali iyapokee na kutafanyia kazi,” alisema Akitoa mfano alisema nchini Uganda hatua za bajeti zimekuwa zikihusisha sekta binafsi ambayo imekuwa ikishiriki kikamilifu maandalizi ya bajeti ya serikali.