Hakimu kesi ya wabunge Chadema augua ghafla

HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Ivan Msack anayesikiliza kesi ya kufanya vurugu inayowakabili Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali na Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga wote kutoka Chadema, ameugua ghafla.

Taarifa za kuugua kwa hakimu huyo zilitolewa jana wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo ili kusikilizwa na kujadili maombi ya kiapo cha dhamana. Kutokana na hatua hiyo, sasa kesi hiyo inayowakabili pia wafuasi 34 wa chama hicho itasikilizwa kesho.

Watuhumiwa wote walifikishwa mapema mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi kwa ajili ya kusikiliza hoja ya maombi ya dhamana iliyopangwa kujadiliwa tena jana. Kesi hiyo iliahirishwa juzi kupisha upande wa Mawakili wa Serikali, kupitia hati iliyowasilishwa na upande wa utetezi, iliyokuwa inataka washitakiwa hao wapatiwe dhamana.

Upande wa wakili wa Serikali ukiongozwa na Sunday Hyera akishirikiana na Edgar Bantulaki, waliiambia mahakama hiyo jana kuwa wako tayari kupitia hati iliyowasilishwa na upande wa utetezi, ambao unaongozwa na Barthlomew Tarimo, akishirikiana na Wakili Peter Kibatala.