Odinga asisitiza kuapishwa Des 12

KIONGOZI wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya (NASA) amezitaka nchi za magharibi zisimuingilie katika mpango wake wa kuapishwa mapema wiki ijayo kuwa rais wa taifa la Kenya.

Alisema Marekani na nchi nyingine zinazojaribu kumshauri aachane na sherehe hizo za uapisho zilizopangwa kufanyika Desemba 12, wanatakiwa watambue kuwa matakwa ya wananchi hayawezi kuzuiwa.

Aliitaka Marekani iache kuzungumzia suala hilo la kuapishwa kwake na kulihusisha na Katiba, kwani nchi hiyo imeshindwa kujitokeza na kuzungumzia mauaji ya wananchi yaliyotokea katika kipindi chote cha uchaguzi nchini humo.

“Tulifikiri tuna marafiki lakini kumbe hatukuwa sahihi, sasa tumejua kuwa ni adui zetu. Hadi leo hii hakuna balozi yeyote aliyejitokeza kulaani mauaji yaliyotokea wakati wa vurugu baina ya Polisi na wananchi,” alieleza Odinga. Alizitaka nchi hizo za magharibi kutojihusisha na matatizo ya Kenya, kwa kuwa matatizo ya nchi hiyo yatatuliwa na Wakenya wenyewe.

Raila aliyasema hayo jijini Nairobi alipokwenda kutoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika kipindi cha uchaguzi. Kiongozi huyo wa NASA alidai kuwa tangu uchaguzi uliofanyika Agosti, mwaka huu, watu 215 wameuawa huku serikali ya Kenya ikiwa kimya.

Hata hivyo, Polisi imekanusha madai ya kiongozi huyo na wafuasi wake na kubainisha kuwa ni watu wachache tu ndio wanaopoteza maisha wakati jeshi hilo likijaribu kudhibiti vurugu zilizoanzishwa katika mitaa mbalimbali nchini Kenya. Wengi wa watu waliopoteza maisha katika uchaguzi huo, walitokea katika mji wa Siaya ambako ndiko anakotokea Odinga pamoja na Kisumu. Kila familia iliyopoteza ndugu ilipewa shilingi za Kenya 50,000 kwa ajili ya kusaidia shughuli za mazishi.