JPM kuboresha benki ya wanawake

RAIS John Magufuli amesema hajaridhishwa na utendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) hivyo ataipitia upya, kuiangalia vizuri na kuichambua.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 9 wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Magufuli alisema wataiangalia vizuri benki hiyo ili iwe katika ushindani wa kibiashara wa kisasa.

Rais Magufuli alisema hajaridhishwa na utendaji wa banki hiyo kwani haijakidhi matakwa ya kuanzishwa kwake ili kusaidia wanawake, lakini kwa bahati mbaya wakopeshwaji wakubwa wa benki hiyo amekuwa si wanawake badala yake wamekuwa wanaume.

Aidha Rais Magufuli alisma benki hiyo haijasambaza matawi katika mikoa mingine nchini, matawi yote ya benki hiyo mengi yapo jijini Dar es Salaam. “Hili la Benki ya Wanawake Tanzania lazima niwaeleze ukweli, haifanyi vizuri nikiwaficha nitakuwa mnafiki, tangu kuanzishwa kwake na mtaji kupewa bado utendaji wake hauridhishi,” alisema na kuongeza:

“Nataka niwaeleze, hata wanaokopa hapo si wanawake na riba ni kubwa kweli kwa wanawake, sasa unakuwa na benki ya wanawake lakini haiwasaidii badala yake inawaumiza wanawake,” alisema.

Rais Magufuli alibainisha kwamba kutokana na hali hiyo watapitia upya na kuichambua vizuri ili iweze kukidhi matakwa ya kuanzishwa kwake. “Tutaichambua vizuri na ndiyo maana mmeona matawi yote ya benki ya wanawake mengi yapo Dar es Salaam pamoja na uwepo wake tulikosa kura Dar es Salaam.

Hili akinamama inabidi niwaeleze maana msema kweli ni mpenzi wa Mungu,” alisema Magufuli Alisema katika taratibu za sasa, benki hiyo ambayo itashindwa kujiendesha kibiashara inafutwa na kwamba hawawezi kuwa na benki ambayo watu wake, wanafanya ufisadi na inaendelea kubebwa wakati inaumiza uchumi wa watu.

Alisema benki yoyote iwe ya serikali au iwe ya wanawake, iwe ya nani, lazima ifanye kazi. Alisema kiukweli benki hiyo ni isiwe chombo cha kuleta hasara katika fedha ambazo zingekwenda kusaidia hospitalini na kusaidia wakulima, badala yake zinaenda kwenye benki ya wanawake kwa jina tu wakati wanaokopa pale kwa asilimia kubwa ni wanaume.

Rais Mafuguli aliwaomba viongozi wapya wa benki hiyo kusaidia katika kufanya uundaji upya wa benki hiyo ili iende sambamba na nia ya kuanzishwa kwake. “Mimi natamani mwanamke apate mkopo wenye riba ya chini itakayomwezesha ili afanye mambo yake vizuri, lakini benki hii imekuwa ikiwanyonya wanawake licha ya kuwa ni ya wanawake,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia suala la asilimia 10 ya mfuko wa Wanawake na Vijana inayotengewa na Halmashauri nchini, Rais Magufuli alimuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kushughulikia ili fedha hizo zitolewe bila kigugumizi.

Uchaguzi wa UWT Wakati huo huo, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliwataka wanachama wa UWT kumchagua mtu ambaye si mtoa rushwa na anayetetea maslahi yao.

“Niwaombe wana CCM na UWT mnafahamu mahali gani tulijikwaa, UWT iliyokuwa ya akina Sophia Kawawa siyo UWT tuliyonayo sasa. UWT tuliyoitegemea siku za nyuma siyo UWT tuliyo nayo sasa.

“Mimi siwezi nikawaficha ni lazima nilipasue jipu moja kwa moja hapa hapa na ndiyo maana ilifika wakati mtu akitaka kuwa kiongozi ni lazima amtafute kiongozi wa UWT ili ambebe hata kama utaenda mahali pengine ataendelea kumbeba,” alisema Magufuli.

Mwenyekiti wa Chama, Rais Magufuli alibainisha kwamba ilifikia mahali viongozi na itikadi na maslahi ya akinamama wa UWT yakaanza kupotea badala ya viongozi kuwachagua kwa sababu wana uwezo wakaanza kuchagua viongozi kwa sababu wana fedha.

“Lazima nilieleze nilipata shida wakati nilipochaguliwa kuwa Rais nilipoanza kutafuta nafasi za kuwateua akinamama hata wale waliokuwa wamegombea kwenye nafasi mbalimbali nilipoangalia kwenye orodha niliyoletewa akinamama wote waliokuwa wamegombea kwenye nafasi mbalimbali wasifu zao hazikuwepo.

“Ilikuwa ni kazi kuchagua mtu ambaye wasifu wake haukuambatanishwa huwezi kujua amemaliza darasa la saba, kidato cha nne, huwezi kujua nini yaliandikwa majina yakakabidhiwa, kiliniuma sana akina mama wengi wenye sifa hawakuweza kuchaguliwa nataka niwaeleze hili ukweli,” alisema.

Mwenyekiti Magufuli aliwataka wanachama wa umoja huo, katika uchaguzi huo, wachague viongozi bila kuangalia amewapa kanga kiasi gani, amewalipia hoteli kiasi gani na anajitangaza anasaidiwa na nani.

“Nataka mchague kwenye dhamira zenu kwa kumtanguliza Mungu, mchague viongozi bora kwa ajili ya akinamama, nataka mchague atakayekuwa mtetezi wa akinamama siyo wa tumbo lake, atakayewaweka pamoja akinamama, nataka anayethamini na kuamini kwa dhati kanuni za CCM na ni kweli nawapenda kweli,” alisema.

Aliwaomba kuchagua kiongozi ambaye kila siku atampeleka sifa za akina mama anaotaka kuwateua na asiye na ubaguzi. Uchaguzi ndani ya chama Rais Magufuli akizungumzia kuhusu uchaguzi ndani ya chama, aliwataka wagombea ambao kura hazikutosha wasikate tamaa wala kuvunjika moyo badala yake wawaunge mkono viongozi waliochaguliwa.

“Natambua kuwa zimetokea kasoro kadhaa za uchaguzi kwenye baadhi ya maeneo chama katika ngazi mbalimbali kinaendelea kushughulikia hilo na ikithibitika kwamba kulikuwepo na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi katika eneo au ngazi yoyote, hatutasita kuchukua hatua na ikilazimu tutarudia uchaguzi kwenye eneo husika,” alisema.

Mwenyekiti alieleza kwamba anataka kuwa na wanachama na viongozi waliopata kihalali na kwa uadilifu mkubwa. “Na wala sizungumzi tu kwa Chama Cha Mapinduzi kupitia UWT, lakini katika ngazi zote iwe Umoja wa Vijana, iwe Wazazi wawe viongozi wenyewe wa CCM, UWT tunakusanya takwimu kwa kila uchaguzi uliofanyika kuanzia huko chini hadi Taifa,” alisema.

Mwenyekiti alieleza kwamba kama kuna watu waliojipenyeza kwa sababu ya rushwa, ikidhihirika kuna mchezo mchafu ulifanyika vikao vya chama vitatoa maamuzi ya kufuta na kuchukua hatua za nidhamu.

“Haiwezekani kuwa na viongozi ambao wamebebwa na mtu mwingine kwa maslahi ya aina fulani au sababu fulani,” alisema Magufuli. Awali, Akisoma taarifa ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Katibu Mkuu, Amina Makilangi alimuomba Rais Magufuli kutoifuta benki hiyo kwamba inapaswa kuongezewa mtaji ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa kuwa bado haijawafikia wanawake hasa wa vijijini.

Alisema pia suala la asilimia 10 inayotakiwa kutengwa na halmashauri kwa ajili ya wanawake na vijana, imekuwa haitolewi na ikitolewa ni kidogo na haifiki kwa wakati na kuomba kutungwa kwa sheria ambayo itazilazimisha Halmashauri kutoa fedha hizo.