Maadhimisho ya Uhuru kufanyika Dodoma leo

LEO ni Siku ya Maadhimisho ya Sherehe ya Miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara yanayofanyika kitaifa mkoani hapa katika Uwanja ya Jamhuri.

Mgeni rasmi katika maadhimisho haya ni Amri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli ambaye pamoja na shughuli nyingine atapokea salaamu za askari waliopo kwenye gwaride, atapigiwa mizinga 21 pamoja na kuimbiwa wimbo wa Taifa na wa Afrika Mashariki.

Rais Magafuli aliyefi ka mjini hapa tangu Desemba 7, mwaka huu anawaongoza mamilioni ya Watanzania katika kusherehekea miaka 56 ya Uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961 na miaka 55 ya Jamhuri.

Katika maadhimisho hayo ya mwaka huu yana kaulimbiu, ‘Uhuru Wetu ni Tunu, tuudumishe, Tulinde raslimali zetu, tuwe wazalendo, Tukemee rushwa na Uzembe, yanafanyika mjini hapa.’

Pamoja na Rais Magufuli viongozi wengine wa kitaifa waliopo katika jukwaa kuu ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi kutoka Zanzibar pamoja na Mawaziri Wakuu wastaafu, David Msuya na Mizengo Pinda.

Pamoja na viongozi hao wa kitaifa, pia wapo viongozi mbalimbali waalikwa kutoka madhehebu mbalimbali ya dini, vyama vya siasa wakiwemo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Miongoni mwa shughuli zinazofanyika leo ni pamoja na gwaride la makamanda wa majeshi ya ulinzi na usalama nchini, maonesho ya vikundi vya makomando na onesho ya kwata ya kimya kimya na gwaride la mkoloni na la wanafunzi.

Pia katika kunogesha maadhimisho hayo, vimealikwa vikundi mbalimbali vya ngoma za asili ili kutumbuiza, kikundi cha kwaya toka Chunya, mkoani Songwe na Tanzania All Stars na vikundi vingine.

Awali akizungumza na vyombo vya habari, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Bilinith Mahenge aliwaalika wananchi wote wa mkoa ya Dodoma na mikoa jirani kufi ka na kuhudhuria kwa wingi katika sherehe hizo.

Dk Mahenge alisema tangu serikali ilipoamua kuhamishia makao makuu mkoani Dodoma, mkoa umepata heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho mbalimbali yakiweno ya sherehe hizo za Uhuru, hivyo wananchi watumie fursa hiyo kuhudhuria kwa wingi.

Maadhimisho ya mwaka jana ya miaka 55 ya Uhuru, yalifanyika mkoani Dar es Salaam na Rais Magufuli alikuwa mgeni rasmi ambapo aliahidi kwamba ya mwaka huu yangefanyika mkoani hapa.