Rais Magufuli awataka UVCCM kujenga 'daraja' kwa vijana wengine

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi John Magufuli amewataka Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kutochagua viongozi kwa kufuata kigezo kingine chochote bali kuweka utaifa mbele.

Rais Magufuli amesema hayo hapa mjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa tisa wa UVCCM ambao utafanyika uchaguzi wa kumpata mwenyekiti na makamu wake pamoja na wajumbe wa umoja huo.

Aidha Rais Magufuli amewataka pia UVCCM kutojenga ukuta kwa vijana wengine ambao wanataka kujiunga na umoja huo ambapo amewaambia waufanye umoja huo kua kimbilio la vijana wa Tanzania.

"Mimi ni Rais lakini sio wa maisha yote, nafasi hizi za uongozi ni zetu vijana lakini tusingependa tunapoondoka tunamuachia kijana mla rushwa," alisema Rais Magufuli. Amewataka pia viongozi watakaochaguliwa kuziorodhesha mali zote za jumuia hiyo nchi nzima na pia kubadilika na kuwa UVCCM mpya yenye vijana uzalendo na wachapa kazi.