Madiwani ‘wanaonunuliwa’ wapashwa

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuacha tabia ya kuwatetea na kuwalinda watumishi wanaotuhumiwa kwa makosa ya ubadhirifu wa mapato ya halmashauri hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamiseni), George Kakunda alitoa onyo hilo wakati akipata taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Onesmo Buswelu alisema kuna baadhi ya watumishi siyo waaminifu kwenye kukusanya mapato na walisimamishwa kazi, lakini Baraza la Madiwani linawalinda na kuwarudisha kazini, jambo linalosababisha halmashauri iendelee kupoteza mapato yake kupitia kwa watu.

Kakunda alisema hiyo ni aibu kwa baraza la madiwani maana watuhumiwa wanapita usiku na kuwapa fedha ili wawatetee, huku mapato ya halmashauri yao yakiwa madogo kutokana na baadhi ya watumishi kutokuwa waaminifu.

Aliagiza mchakato wa hatua za kinidhamu kwa watumishi waliosimamishwa kazi kwa tuhuma hizo urudiwe, kwa Mkurugenzi Mtendaji Valerian Juwal, kupeleka tena jambo hilo kwenye baraza na kama kuna diwani atatetea wamjue na aeleze amelipwa shilingi ngapi.