Samia: Njooni muone tunavyoondoa rushwa

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imepiga hatua kubwa dhidi ya vita vya rushwa na kuwataka waliokuwa wakisema kuwa nchi hii haiwezi kudhibiti rushwa waje waone.

Alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya maadili na haki za binadamu nchini viwanja vya Mwalimu Nyerere mjini hapa. Alisema Tanzania imeshika nafasi ya 16 bora Afrika kwa upambanaji na rushwa jambo ambalo linatia moyo kushuka kwa rushwa.

“Waliosema Tanzania hawawezi kudhibiti rushwa waje watutazame,” alisema. Pia aliwataka wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa vitendo vya na jitihada za Serikali kuziba mianya ya upotevu wa rasilimali za nchi, mapato na mapambano dhidi ya rushwa.

Alisema lengo ni kuunganisha nguvu ya pamoja kusimamia maadili ya taifa na utawala bora. Alisema ajenda kubwa duniani kwa sasa ni kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha utawala bora unaobeba mambo mengi muhimu kama utawala wa sheria, haki za binadamu, maadili, uwazi na uwajibikaji.

Alisema Serikali imekusudia kuona Tanzania inapata maendeleo kwa manufaa ya wananchi. “Kufikia azma hii si suala dogo. Lazima wananchi na Serikali kwa ujumla kujizatiti kutekeleza dira ya maendeleo ya taifa ya 2025 na ilani ya uchaguzi ya chama tawala 2015/2020 inayolenga kuiwezesha nchi yetu kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda," alisema.

Alisema juhudi hizo haziwezi kufanikiwa wasipodhibiti rushwa na kusimamia uadilifu na uwajibikaji ipasavyo. "Hatutasita kuwachukulia hatua wale wote watakaotukwamisha kufikia azma hiyo," alisema Mama Samia.

Alisema vita dhidi ya ukiukwaji wa maadili haviwezi kupiganwa na Serikali peke yake ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha rushwa, ubadhirifu na maovu mengine vinatokomezwa.

"Ni vyema tukahimizana suala la kuzingatia maadili na haki za binadamu ili kufikia malengo ya kuwa taifa la mfano duniani, matatizo yanayowakabili Serikali ni pamoja na matumizi mabaya ya nyaraka za siri za Serikali,” alisema.

Alisema kukabiliana na changamoto ya maadili nchini Serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kisera na kisheria ambayo itahakikisha vijana wanakuzwa kimaadili kwani hakuna taifa duniani linaloweza kupata maendeleo bila utamaduni unaozingatia maadili.

"Kuna mtindo wa baadhi ya ofisi za Serikali kufanya kazi zao bila kufuata utaratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya huduma kwa wateja na dhamira ya Serikali ya kutoa huduma bora, hali hii inayotokana na kuchukua muda mrefu kutekeleza wajibu wao au kurudisha mrejesho kwa wananchi na hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi.

Alisema huduma zinazotolewa ni vyema zikaainishwa bayana muda utakaotumika na vigezo vinavyohitajika. "Serikali hii inataka viongozi wanaotimiza wajibu wao kwa wakati, vijana wenye mioyo na ari ya kazi hivyo kama kuna mtu mzembe viongozi msisite kuwaondoa,” alisema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), Dk Valentino Mlowola alisema watatekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwani kwa kufanya hivyo wananchi wanajenga imani na Serikali.