Shambulio lililoua askari halina mfano -JWTZ

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema shambulizi lililotokea Desemba 7, mwaka huu dhidi ya askari wake wanaolinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni baya na halijawahi kutokea tangu vikosi vyake vianze kushiriki Ulinzi wa Amani huko kupitia Umoja wa Mataifa mwaka 2011.

Kutokana na shambulio hilo lililodumu kwa saa 13, JWTZ imepoteza askari 14 na wengine 44 wamejeruhiwa, wawili wakiwa hawajulikani walipo na jitihada za kuwatafuta zinaendelea.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa alisema shambulio lililotokea DRC ni shambulio ambalo kwa mara ya kwanza jeshi hilo liliamua kutoa taarifa. Alisema shambulio hilo limeleta madhara makubwa lakini kikosi chao kilichopo huko bado kina uwezo wa kutekeleza majukumu kwa uhodari, ushupavu, weledi na umahiri stahiki.

“Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini DRC, Tutawakumbuka daima mashujaa wetu hao,” alisema Kamanda huyo. Alisema taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha nchini zinafanyika chini ya utaratibu wa Serikali na Umoja wa Mataifa. Alisema taratibu za kuwajulisha familia za wafiwa zimekamilika ndiyo maana hawakuweza kutoa taarifa hizo bila kuweka sawa familia zao.

Alisema kutokana na shambulio hilo, JWTZ na Serikali zinaendelea kuchukua hatua stahiki ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika. “Kwa umoja wetu Watanzania tuombee dua roho za mashujaa wetu zipumzike kwa amani na majeruhi wetu wapone haraka iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao,” alisema.

Desemba 07, mwaka huu jioni sehemu ya Kikosi cha askari wa JWTZ kilichopo DRC kulinda amani kilivamiwa na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika kambi ndogo iliyopo eneo la daraja mto Simulike barabara ya kutokea Oicha kwenda Kamango mpakani mwa Uganda Kaskazini Mashariki ya Wilaya ya Beni, jimbo la Kivu Kaskazini. Hata hivyo, shambulio hilo la kuvizia lilizusha mapigano baina ya kikosi cha JWTZ na waasi hao ambapo askari wa JWTZ waliuawa na wengine kujeruhiwa vibaya. UN imethibitisha.