Kigogo UVCCM kizimbani kwa rushwa, anyimwa dhamana

SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kurudia kukemea vitendo vya rushwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis jana alipandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Mkoa wa Dodoma, akikabiliwa na makosa mawili yanayohusu rushwa.

Sadifa, baadaye alinyimwa dhamana kwa madai ya kuhofia kuingilia uchaguzi. Mshtakiwa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Zanzibar, alifikishwa Mahakamani hapo majira ya saa 4:45 asubuhi na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) akiwa katika gari lenye namba za usajili T994 BEM.

Akisoma kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Joseph Fovo, Wakili wa serikali kutoka Takukuru, Biswaro Biswaro alisema katika kesi hiyo ya jinai namba 232 ya mwaka 2017, mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Desemba 9, mwaka huu akiwa nyumbani kwake maeneo ya Kata ya Mnadani Manispaa ya Dodoma.

Alisema katika kosa la kwanza, Sadifa anadaiwa kuwa akiwa nyumbani kwake alitoa rushwa ya vinywaji kwa wajumbe ili wamchague mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Rashid Mohamed Rashid.

Biswaro alisema kosa la pili analokabiliwa nalo Sadifa ni kutoa ahadi ya kuwalipia gharama za usafiri wajumbe hao kutoka Dodoma –Kagera kama zawadi kwao baada ya kumpigia kura mgombea huyo.

Wakili huyo aliwataja wajumbe hao kuwa ni Kadogo Shaaban, Abdallah Hamimu, Octavian Andrea, Didas Zimbihile, Tasinta Nyamwiza, John Lufunga, Mtwawafu Kantangayo, Haleluya Ivody, Deocres Kagunila, Emmanuel Shitobelo, Happiness Rinyogote, Adolf Andrew, Adinani Musheruzi, Editha Domician na Hashim Abdallah.

Biswaro alisema mshitakiwa huyo, alitenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 Kifungu cha 15(1)(b) na (2). Alisema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na upande wa Jamhuri unaweka pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Fovo alimhoji mshtakiwa huyo ambapo alikana kutenda makosa yote mawili. Kukosa dhamana Wakili Biswaro alisema sababu za kuzuia dhamana ya mshitakiwa huyo kutokana na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi UVCCM ni wa siku mbili mfululizo Desemba 10 na 11, 2017 na matokeo bado hayajatangazwa, hivyo kuna uwezekano wa kuingilia uchaguzi huo.

“Naomba Mahakama itambue uchaguzi bado unaendelea na mshitakiwa hadi sasa hajakabidhi uongozi bado ni mwenyekiti,” alisema Aidha, alisema sababu nyingine ni kuwa mashahidi wengi ni viongozi ambao ni Mwenyekiti na Makatibu; na endapo akiachiwa kwa dhamana, ana kila aina ya ushawishi anaweza kuvuruga upelelezi.

Kufuatia maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Godfrey Wasonga alipinga kuzuiwa kwa dhamana na kudai kuwa ni haki ya mtu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kiapo cha kuzuia dhamana hicho kilichowasilishwa mahakamani, ambacho kimetolewa na Emma Kuhanga (Kamanda wa Takukuru Dodoma) hakina mashiko. Alisema Uchaguzi wa UVCCM umeshaisha na mshindi tayari ameshapatikana na hakuna uchaguzi mwingine wa kuingilia au kama kuna uchaguzi utafanyika kiapo kingesema.

Alihoji sababu za kupelekwa kesi ambayo haijakamilika upelelezi na kuzuia dhamana kwa mshtakiwa na kwamba mshtakiwa huyo hataweza kuingilia uchunguzi kwa sababu walizozitoa. “Mteja wangu ni mbunge ni mtu makini na anaaminiwa asihukumiwe kwa kuwekwa ndani kwa sababu zisizo na mashiko,” alisema Wasonga.

Aliomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hilo na mshtakiwa apewe dhamana kwa kuwa hataweza kuingilia uchaguzi na uchaguzi mwingine wa Umoja huo ni hadi mwaka 2022.

Kufuatia mvutano huo, Hakimu Fovo aliahirisha kesi hiyo hadi desemba 19, mwaka huu na kwamba Mahakama ndipo itatoa maamuzi kuhusu suala hilo na mshtakiwa ataendelea kuwa rumande