Kagame ataja mbinu kuinua uchumi Afrika

RAIS wa Rwanda, Paul Kagame ametoa mwito kwa nchi za Afrika, kuboresha mazingira ya biashara sanjari na kuongeza kasi ya mtangamano ili zifanikiwe kiuchumi kupitia sekta binafsi.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo kutoka moja ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika siku zijazo maendeleo na ukuaji uchumi barani humo utaitegemea zaidi sekta hiyo, hivyo ni muhimu kumaliza masharti yasiyo ya lazima na ucheleweshaji usio na umuhimu ili kuwa na mazingira bora ya biashara.

Mbali ya Rwanda, nchi nyingine za EAC ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini. Alitoa changamoto hiyo mwishoni mwa wiki, Sharm el Sheikh, nchini Misri wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Biashara Afrika 2017 wenye lengo la kukuza uwekezaji ndani ya nchi za Afrika sanjari na kuongeza ushirikiano kuvuka mipaka.

Ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu ulihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Guinea, Alpha Conde, Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed, na Katibu Mkuu wa COMESA, Sindiso Ngwenya.

“Bara letu lifanye haraka na lishindane kidunia. Hatuwezi kuendelea kupoteza fursa kwa sababu ya masharti yasiyo na umuhimu yanayoendana na ucheleweshaji,” alisema Rais Kagame.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mazingira ya biashara yanaweza kuboreshwa zaidi kwa kuongeza kasi ya mtangamano ili kuwa rahisi kwa nchi hizo kufanya biashara baina yao na kuvutia uwekezaji.

“Ndiyo maana ushirikiano kwenye eneo hili unakuwa jambo la msingi kwa hali ya baadaye ya Afrika. Kama tunavyoona kwa kusainiwa kwa makubaliano ya eneo huru la biashara la utatu (TFTA) mwaka 2015 hapa Sharm El Sheikh unaounganisha COMESA (Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika bila kutaja eneo huru kubwa la biashara la bara likiongozwa na Umoja wa Afrika,” alisema Rais Kagame.

Alisema, mchakato unaoendelea wa mageuzi kwenye Umoja wa Afrika utaongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano hayo. Katika ufunguzi huo, Rais Kagame pia alizungumzia umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ya kisasa ili kuongeza muingiliano.

Alisema mambo hayo yaachwe kwa vijana hususan wajasiriamali. Kwa mujibu wa Rais Kagame, uchumi uliofanikiwa ni ule wenye uelewa Awali, Rais Kagame aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa, rasilimali watu iliyopo Afrika ina thamani zaidi kuliko madini yote na mafuta yaliyomo barani humo.

Alisema, vijana wanaweza kuwa injini ya mafanikio Afrika kama watajengewa mazingira watumie uwezo walionao. Alitoa mfano wa Rwanda kwamba, nchi hiyo imetengeneza mfumo unaohusisha uelewa, ujuzi, na taasisi.

Kwa mujibu wa Rais Kagame, jambo la msingi si kuhesabu idadi ya watu barani Afrika ila kutathmini uwezo wao na kujenga mazingira ili watumie ipasavyo vipawa vyao. “Bara letu ni maarufu kwa mali asili zake lakini thamani ya mtaji wa watu tulionao, watu wetu, inazidi mafuta yote na madini kwenye bara hili,” alisema kiongozi huyo anayejiandaa kuwa Mwenyekiti wa AU.

Mkutano huo wa pili wa biashara Afrika umehudhuriwa viongozi mbalimbali Afrika wakiwemo wakuu wa nchi na serikali, na wakuu wa kampuni na mashirika barani humo. “Rwanda tumetengeneza mfumo wa utatu, uelewa, ujuzi na taasisi ambako unaona teknolojia ikitumika… hizi taasisi zinatoa mawazo ambayo yanageuka kuwa biashara au bidhaa.

Tumelifanya hili kwa namna ambayo haisaidii Rwanda tu, lakini pia taasisi za kimataifa zenye makao Rwanda,” alisema Rais Kagame. Mfumo mwingine unaotumiwa na Rwanda kutumia vipaji na uwezo wa vijana unahusisha elimu ya juu ikiwemo ya ufundi na mafunzo na elimu ya ufundi stadi (TVET) vinavyotoa takribani wahitimu vijana 90,000 kila mwaka.

Rais Kagame ametoa mwito kwa nchi na wajumbe kwenye mkutano huo kudhamiria kutengeneza fursa kwa vijana wao. “Rwanda inatengeneza mfumo utakaonufaisha wajasiriamali Waafrika.

Tudhamirie kwa nafasi zetu kutengeneza fursa kwa vijana Waafrika,” alisema na kutoa mwito kwa vijana kufanya kazi kwa bidii na wasiogope kujaribu. “Vijana na kila mmoja anayehusika, tunatakiwa kuwa kwenye ubora wetu, ni jukumu letu, jamii zetu na bara kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kujaribu, tusiache kujaribu…” alisema Rais Kagame.

Wazungumzaji wakuu wengine kwenye mkutano huo ni pamoja na Rais wa Misri, Al Sisi, mfanyabiashara bilionea wa Nigeria, Tony Elumelu na mabalozi wajasiriamali vijana, Jean Bosco Nzeyimana, na Mohamed Azab.