Siasa kikwazo uchumi Afrika – Museveni

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amesema, uchumi wa mataifa mengi ya Afrika unakwama kwa sababu ya msisitizo unaowekwa zaidi kwenye siasa za utambulisho kuliko maslahi ya nchi hizo.

Kiongozi huyo ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kuwa, kosa hilo ni kubwa na lazima litafutiwe ufumbuzi. Rais Museveni ni miongoni mwa wakuu wa nchi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wenye bidii ya kutumia mtandao wa kijamii wa twitter kuwasiliana na jamii ikiwa ni pamoja na kutuma mrejesho wa yanayotokea kwenye matukio anayoshiriki zikiwemo picha.

Alijiunga kwenye mtandao huo Machi, 2010, kuna watu 648,798 wanaomfuatilia na yeye anawafuatilia watu 25. “Sehemu ya tatizo la Afrika ni kwamba, wana mtazamo mmoja wa kutatua matatizo.

Kwenye miaka ya 1960 kama ulihudhuria semina kuhusu Afrika walizungumzia kuhusu maendeleo ya uchumi vijijini na baadaye kwenye miaka ya 1970 walibadilisha kwenda kwenye elimu na ukombozi wa wanawake.

Mara nyingi hili halikuwa na chochote,” alisema Rais Museveni kwenye ukurasa huo. Kwa mujibu wa Museveni, ukiwa na itikadi au mtazamo potofu huwezi kujenga mihimili ya nchi au taifa kama vile jeshi kwa sababu unafikiria makabila na utaishia kuwa kama nchi za Somalia au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zinazoagiza ulinzi kutoka mataifa ya nje.

Kwenye ukurasa huo, alisema matatizo ya kisiasa ya washirika wa biashara wa Uganda yamesababisha kushuka kwa bei bidhaa ikiwemo chai, nyama na maziwa. “Bei ya chai iliathiriwa na matatizo Misri, bei ya nyama kwa matatizo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na maziwa kwa matatizo Sudan Kusini,” aliandika Rais Museveni.

Kwenye ukurasa huo, kiongozi huyo alitaja matatizo mengine yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi nchini humo kuwa ni miundombinu. Kwa mujibu wa Rais Museveni, kutoendeleza miundombinu inamaanisha gharama kubwa za umeme na usafirishaji, na kupungua kwa faida katika sekta binafsi kwa sababu ya gharama kubwa za malighafi.

“Baada ya kushughulikia tatizo la umeme, Serikali sasa inatatua suala la gharama kubwa za usafirishaji kwa kujenga reli na kuiunganisha kwenye maziwa,” alisema kwenye kurasa huo. Rais Museveni amesema, mizigo lazima isafirishwe kwa reli na maji, na kwamba, na barabara ziachwe kwa ajili ya watu.

“Baada ya kumaliza suala la usafirishaji, hatari pekee inayobaki itakuwa rushwa na uchelewaji kwenye kufanya uamuzi,” alisema. Kwenye ukurasa huo alitaja tatizo lingine kuwa ni kuisaidia sekta binafsi na kuliunganisha soko lililogawanyika kwa sababu ya ukoloni.

Alisema, mara nyingi Uganda haibughudhi wawekezaji kwa kodi, na kwamba, inachotaka ni kutumia malighafi zake, kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa nje na kutengeneza ajira kwa Waganda. “Uganda ipo imara na ina amani sana.

Pia tuna miundombinu ya kutosha kama barabara na umeme. Tunajenga mtandao wa kisasa wa reli,” alisema Rais Museveni. Alisema, mahitaji Afrika yanaongezeka kwa sababu imekuwa na mahitaji ya chini wakati yanapungua maeneo mengine kwa sababu wamekuwa wakitumia kupita kiasi.

Rais Museveni amesema, Uganda ina malighafi nyingi, na watu takribani milioni 40. “Ukiunganisha kwenye EAC na COMESA (Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika), idadi inaongezeka hadi watu milioni 600,” alisema Rais Museveni kwenye ukurasa huo