Kenya nao waja kujifunza mradi mabasi ya haraka

SIKU chache baada ya Rwanda kutuma ujumbe wake Dar es Salaam kujifunza juu ya uendeshaji wa usafi ri wa mabasi ya haraka mijini, Kenya nayo imefanya hivyo kwa kutuma ujumbe wa watu 16.

Wataalamu kutoka Mamlaka ya Usafirishai wa Jiji la Nairobi (NAMATA) nchini Kenya, tayari wapo Dar es Salaam na wamebainisha kuwa na mpango wa kuanzisha huduma ya mabasi yaendayo haraka, mradi utakaosaidia kuunganisha miji mitano nchini humo.

Akizungumza jana wakati wa ziara ya mafunzo kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NAMATA, James Ng’ang’a alisema kutokana na kuwa na mpango huo wameona waje nchini Tanzania kujifunza namna mradi huo unavyofanya kazi kabla ya kuanza kutekeleza mradi wao.

“Tumekuja kujifunza Tanzania namna ya kuendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka kwa kuangalia changamoto mlizokutana nazo, mafanikio mliyoyapata ili nasi tuwe na utekelezaji mzuri wa mradi kama huu.”

“Tumechangua kuja Tanzania kwa sababu ni eneo la karibu kwetu, lakini sababu kubwa ni kutokana na kuwa Tanzania imetekeleza mradi huu kwa muda mfupi na kuwa na mafanikio makubwa,” alisema.

NAMATA ni muunganiko wa miji mikuu mitano ya Kajiado, Nairobi, Machakos, Murang’a na Kiambuu ambayo imelenga kuanzisha huduma ya Mabasi ya mwendokasi katika miji hiyo.

Jopo la wataalamu 16 kutoka NAMATA wako nchini kwa ziara ya siku nne ya kujifunza namna mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka unavyofanya kazi. Katika siku za hivi karibuni, Wakala umepokea wataalamu waliokuja kujifunza namna mradi huo unavyofanya kazi kutoka nchi za Rwanda, Zambia, Uganda, na Ethiopia.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), John Shauri alisema huduma ya usafiri inayotolewa tangu mradi huo kuanza kufanya kazi umeweza kusafirisha watu 200,000 kila siku na kupunguza muda wa usafiri kutoka saa nne hadi dakika 45 kutoka Kimara hadi Kivukoni.

Akizungumzia ziara ya wageni kutoka Kenya, Shauri alisema kuwa Wakala unafurahia ziara hizo kwani taasisi hiyo kwa sasa imekuwa kama shule kwa miji na majiji mbalimbali barani Afrika yanayotaka kujifunza kuhusu usimamizi na uendeshaji wa mradi huo.