Marekebisho uwiano wa mishahara yaiva

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amewahakikishia watumishi wa umma kuwa Bodi ya Mishahara na Maslahi (HSRB) iko katika hatua za mwisho za kurekebisha mfumo mzima wa mishahara, utakaondoa tofauti ya uwiano wa mishahara katika taasisi za umma.

Mkuchika alisema kwa miaka mingi wafanyakazi wa umma wenye ujuzi, sifa na uzoefu sawa wamekuwa wakilipwa tofauti kulingana na ofisi anayofanyia kazi. Alisema bodi inaendelea kushughulikia suala hilo na hivi karibuni watumishi wa umma wataambiwa maendeleo yake. Waziri alikuwa akizungumzia mafanikio ya wizara yake katika kipindi cha miaka miwili kupitia kipindi maalumu cha Tunatekeleza kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1).

Mkuchika alisema kazi ya bodi hiyo itakapokamilika, itawasilisha mapendekezo yake serikalini ili hatua zaidi zichukuliwe. Kwa mujibu wa Waziri huyo, watumishi wa umma wanatakiwa kutulia na kusubiri kuona kitakachowasilishwa katika Bunge lijalo la bajeti na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

“Mawaziri wataeleza umma hatua zitakazochukuliwa kuuwianisha mishahara na maslahi kulingana na ushauri na mapendekezo ya ripoti, yatakayowasilishwa na HSRB,” alisema. Aliongeza kuwa kwa muda mrefu wafanyakazi wa umma wamekuwa wakilalamika juu ya mishahara mikubwa wanayolipwa baadhi ya wafanyakazi kwenye taasisi za umma. Alifafanua kuwa, bodi imepewa kazi kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote wa umma wanapata ujira kulingana na viwango vya elimu na hali ya kazi.

Kuhusu mikataba ya wafanyakazi, Waziri alisema ofisi yake haiungi mkono mfumo wa kazi kwa mikataba na kuongeza kuwa mfumo huo ni gharama kubwa ukilinganisha na kuajiri mfanyakazi kwa ajira ya kudumu. Waziri Mkuchika alisema wizara yake inashughulikia suala hilo na kwamba hivi karibuni taasisi za umma hazitaruhusiwa kuajiri wafanyakazi wapya kwa mfumo wa mikataba.

“Tunataka kila ofisi kuajiri kwa mujibu wa mahitaji, hatutaruhusu mfumo huu wa mikataba kuendelea kwa sababu ni gharama kubwa mno kwa serikali,” alisema. Akizungumzia wafanyakazi wa umma wanaokwenda likizo maalumu, Waziri alisema yeyote atakayekwenda katika likizo ya namna hiyo atatakiwa kuwasilisha nyaraka zake wizarani lini anarudi. Alisema wale watakaowasilisha barua kuwa wamerudi wanatakiwa kusubiri jibu la serikali.

“Kama ulikuwa nje ya nchi au ofisi mfano miaka mitano, ni dhahiri kuna mtu alijaza nafasi yako, hivyo unaporudi, unatakiwa kuwasilisha barua na kuipa nafasi serikali kujibu,” alisema. Kwa mujibu wa Mkuchika, likizo maalumu sio jambo jipya katika mfumo wa utumishi wa umma na umekuwa ukitumika katika nchi nyingi duniani. “Sio kwamba ni jambo jipya, wanaondoka katika vituo vyao vya kazi kwa ruhusa, hatuna shida nayo lakini tunataka wafuate taratibu sahihi wanaporudi,” alisema.

Kuhusu Utawala Bora, Waziri Mkuchika alisema hadi sasa serikali inafanya vizuri lakini vita dhidi ya rushwa bado ni changamoto katika mfumo mzima. Alisema ili taifa kulimaliza tatizo lote hilo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) inahitaji kujikita katika kutoa elimu kwa umma.

“Tunahitaji kujifunza kutoka nchi za Scandinavia, wamefanikiwa kupambana na rushwa kwa sababu ya kushirikisha umma, kupitia njia ya uhamasishaji, watu walifundishwa umuhimu wa kupambana na rushwa katika ngazi zote, TAKUKURU inatakiwa kuchukua mkakati huu,” alisema.

Alisema wizara yake tayari imeshajadiliana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi ya namna somo kuhusu rushwa na kuingiza katika muhtasari wa masomo ya shule ya msingi hadi chuo kikuu. “Huwezi kumfundisha mtu kuchukia rushwa akiwa chuo kikuu, tunahitaji kuanzia chini,” alisema.