Madaktari 6 waanza uchunguzi wanafunzi pacha walioungana

JOPO la madaktari sita wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) likiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi, limeanza tiba na uchunguzi wa afya ya pacha walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti (22)waliofi kishwa hapo siku saba zilizopita kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Profesa Janabi alisema tangu kufikishwa kwao hospitalini hapo, uongozi wa JKCI uliunda jopo la madaktari hao watakaofanya kazi kwa pamoja ya kuwachunguza pacha hao kwa lengo la kubaini undani wa tatizo linalowasumbua.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, ujio wa pacha hao ambao ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa mwaka wa kwanza katika hospitali hiyo umetokana na rufaa kutoka mkoani Iringa, huku ikielezwa kuwa tatizo linalowasumbua kuwa ni ugonjwa wa moyo ambalo wanalifanyia uchunguzi ili kulibaini kama ni kweli au la.

“Waliletwa hapa JKCI kutokana na ukubwa wa taasisi hii, tunaamini kuwa tutalishughulikia tatizo lao na kulipatia ufumbuzi kwa asilimia zote bila kuhitaji rufaa kwenda nje ya nchi, na hata kama ikibainika kuwa wana tatizo jingine tofauti na ugonjwa wa moyo, tutashirikiana na wenzetu wa hospitali ya Muhimbili ili kulipatia ufumbuzi,” alisema Prof. Janabi.

Alisema kwa sasa hali za pacha hao inaendelea vizuri wakiwa chini ya usimamizi na uangalizi wa karibu wa mlezi wao, Francisca Malangwa waliyesafiri naye kutoka mkoani Iringa baada ya kupewa rufaa hiyo ya kwenda katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) Alisema kwa kuanza, jopo hilo limefanya uchunguzi wa kina wa kuangalia mifumo ya mwili ya pacha hao, ili kufahamu kwa kina kabla ya kuendelea na hatua zingine zenye lengo la kutoa matokeo chanya ya afya zao.

“Ni mara ya kwanza kwa pacha hawa kufika katika taasisi yetu, kama mtakumbuka vizuri hawa walizaliwa katika mkoa wa Iringa na matibabu yao kwa asilimia kubwa walikuwa wakiyapata kutoka hospitali za mkoa, hivyo ujio wao katika taasisi hii tunaupokea kama kwa namna ya kipekee,” alisema Profesa Janabi.