Machinga waandamana hadi CCM

WAFANYABIASHARA wadogo (machinga) waliopo pembezoni mwa barabara Kuu katikati ya Mji wa Kahama juzi, wameandamana hadi katika ofi si ya wilaya ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wamefanya hivyo ili kupinga kitendo cha Halmashauri ya Mji wa Kahama, kuwaondoa katika maeneo yao waliyokuwa wakifanyia biashara. Wamachinga hao wamekuwa wakifanya biashara zao pembezoni mwa barabara hiyo kwa muda mrefu huku wakiwazuia watembea kwa miguu kupita kwa urahisi kutokana na bidhaa zao nyingi kuwa katika barabara na hivyo kuhatarisha hali ya usalama kwa watembea kwa miguu.

Wakizungumza na gazeti hili katika ofisi za CCM za Wilaya, wafanyabiashara hao walisema kuwa kitendo cha Halmashauri ya Mji wa Kahama kuwandoa katika maeneo yao ya biashara siyo ya kiungwana, kwani hawakuwa na taarifa yoyote juu ya hatua hiyo.

Walisema kuhamishwa kutoka kwenye maeneo yao na kupelekwa katika eneo maarufu la CDT, ambalo limekuwa changamoto ya msongamano wa magari na wafanyabiashara wengi wa biashara ya chakula huku wao wakiuza viatu na nguo, kumekuwa kwa ghafla mno.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Thomas Mnyoga alisema kuwa vijana wengi wanakiamini chama na kuitaka Halmashauri ya Mji wa Kahama kutofanya kazi bila ya kuwaandaa watu, ikiwemo kuwashirikisha katika maamuzi yoyote wanayoamua hususani katika vikao vyao kama vya mabaraza ya madiwani.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema baada ya kusikia malalamiko hayo, alimuita Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhil Nkurlu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba na kukaa kikao kilichodumu kwa saa moja na kushauriana juu ya tatizo hilo na kufikia maelewano mazuri. Msumba alisema kuwa eneo walilohamishiwa wamachinga hao, lina watu wengi, ambalo ni kituo cha mabasi yaendayo mikoani na wangeweza kufanya vizuri biashara.