Majaliwa: Songea limeni kahawa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wajikite katika kuzalisha zao la kahawa ili wawe na zao mbadala la biashara litakalowasaidia kuinuka kiuchumi.

Alitoa wito huo juzi wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lipokela na vijiji jirani, wilayani Songea mara baada ya kukagua shamba la kahawa la Aviv Tanzania lenye ukubwa wa hekta 1,990.

“Limeni kahawa ili mpate fedha sababu zao hili ni la biashara. Kahawa ni miongoni mwa mazao matano ya biashara ambayo Serikali ya awamu ya tano imeamua kuyawekea mkazo ili yaweze kuongeza tija kwa wakulima na kuinua uchumi wa Taifa,” alisema.

“Tumeamua kuweka mkazo kwenye mazao matano ya pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku kwa sababu yanaleta tija na kuliingizia Taifa fedha za kigeni…tumefanya tathmini na tumegundua udhaifu mkubwa katika usimamizi wa mazao haya ndani ya Serikali kuanzia ngazi ya Halmashauri,” alisema.

Alisema ni lazima wananchi walime zao hilo na viongozi wahakikishe linanufaisha wananchi. Alieleza kutoridhishwa na utendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea baada ya kuelezwa kampuni ya Aviv Tanzania imezalisha miche milioni moja lakini iliyochukuliwa na kusambazwa kwa wananchi ni 200,000.

“Kampuni hii imeamua kutoa miche ya bure kwa wakulima, wamezalisha miche milioni moja lakini hadi sasa imechukuliwa 200,000 tu. Kuna miche zaidi ya 800,000, imebaki, na tena wawekezaji hawa wanatoa elimu bure ya kulima na kuitunza mikahawa yako,” alisema Waziri Mkuu akioneshwa wazi kukerwa.

Aliwataka wakulima hao watenge ekari moja hadi tatu kwa kila kaya zilime zao hilo na ikibidi kahawa iundiwe mfumo maalumu wa ununuzi wa ushirika kupitia vyama vya msingi (AMCOS) vilivyokuwepo