Bodaboda zageuzwa mabasi ya wanafunzi

BAADHI ya shule zinazofundisha kwa mchepuo wa Kiingereza Dar es Salaam, ambazo kwa kawaida hutoa huduma ya usafiri kwa wanafunzi, zimebainika kutumia usafiri wa pikipiki kuwasafirishia wanafunzi kurudi majumbani, wakati mabasi ya kuwabeba yanapoharibika.

Uchunguzi wa gazeti hili, uliofanyika kwa kuzitembelea shule mbalimbali, na pia ufuatiliaji kwenye maeneo kadhaa hasa nyakati za asubuhi na mchana, muda ambao wa wanafunzi hupelekwa shule na kurejeshwa majumbani mwao. Katika ufuatiliaji huo, limebaini uwepo wa wanafunzi wakipakiwa kwenye usafiri wa bodaboda huku wengine wakiwa wamepakiwa zaidi ya mwanafunzi mmoja, maarufu kama mshkaki.

Kitu ambacho kinashangaza zaidi ni kuona wanafunzi hao, ambao wengi wao umri wao ni miaka minane hadi 13, umri ambao ni hatarishi kutumia usafiri huo. Lakini pia gazeti hili limebainisha watoto hao kupakiwa kwenye bodaboda hizo, bila hata ya kuvaa kofia ngumu (helmet), kitu ambacho ni hatari zaidi kwa usalama wao.

Ufuatiliaji wa kina wa HabariLeo, umebainisha kuwa kupakiwa kwa wanafunzi hao kwenye bodaboda, kunatokana na shule kushindwa kuwa na mbadala wa mabasi pindi mabasi yakipatwa na hitilafu na kusababishwa kuegeshwa.

Kwa kanuni za uendeshwaji wa shule hizo, inatakiwa kuwepo kwa mabasi mbadala pindi mabasi ya wanafunzi yakikumbwa na hitilafu. Kutokana na uchunguzi huu, gazeti hili lilimtafuta Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni kwa ajili ya ufafanuzi na alisema kuwa ni kosa kisheria kwa mtoto chini ya miaka tisa (9) kupakiwa kwenye bodaboda na tena hasa ikiwa kwa staili ya kupakizana wawili, mshikaki.

Alibainisha, kanuni ya leseni na usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu (Sumatra) ya mwaka 2010, sehemu ya 4 kifungu cha 14, kifungu kidogo cha kwanza kinakataza ubebaji wa watoto walio chini ya miaka 9 katika bodaboda wakiwa kama abiria.

“Moja ya changamoto ambazo kikosi cha usalama wa barabarani inaendelea kukabiliana nazo ni ubebwaji wa watoto kwenye bodaboda, hii sio lazima wale wanaovaa sare za shule, lakini hata akiwa kwenye nguo za nyumbani mtoto chini ya miaka tisa ni marufuku kupanda bodaboda,” alisema Sokoni.

Gazeti hili lilizungumza na mzazi ambae mtoto wake anasoma kwenye moja ya shule hizo iliyopo Tabata, Irene Ngwale ambae alielezea kuhusu watoto ambao hupanda bodaboda hasa wakati wa kwenda shule, ambapo alisema kuna wakati kama mzazi hulazimika kumchukulia mwanawe bodaboda.

Alitolea mfano kuwa kuna wakati mtoto anakuwa ameachwa na basi la shule kutokana na kuchelewa kuamka hivyo hulazimika kumkodishia bodaboda ili awahi shuleni. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Watoaji wa Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara, CIEPSSA, Benjamin Nkonya, aliwataka wamiliki wa shule kuacha mara moja mchezo huo wa kuwapakia wanafunzi kwenye bodaboda na kuwataka kuwa na usafiri mbadala. “Wazazi ambao watoto wao watapandishwa kwenye bodaboda ili hali wamelipia fedha za usafiri wa watoto wao shuleni watoe taarifa kwetu ili tuchukue hatua za haraka,” alisema Mkunya.