Mpina ataifisha tani 65 za samaki wa milioni 300/-

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametaifisha tani 65.6 za samaki aina ya Kayabo wenye thamani ya Sh milioni 300 waliovuliwa kinyume cha sheria katika Kisiwa cha Rubili kilichopo wilayani Muleba mkoani Kagera wakiwa tayari kutoroshwa kwenda nchi za Rwanda na Uganda.

Ameamuru samaki hao wauzwe kwa mnada wa hadhara huku akisisitiza kuwa, wafanyabiashara wenye leseni halali za kusafirisha mazao ya uvuvi nje ya nchi ndio watakaopewa kipaumbele katika mnada huo. Akizungumza mjini Bukoba walikohifadhiwa samaki hao jana, Waziri Mpina alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dk Yohana Budeb, kuwapa wiki mbili wenye leseni za usafirishaji wa samaki na mazao yake kuhuisha leseni zao kwa kuwaongezea masharti mapya.

Miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na kuambatanisha taarifa zao za ulipaji kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusisitiza kuwa, watakaoshindwa kukidhi masharti hayo mapya, wafutiwe leseni zao na wasiruhusiwa kujihusisha na biashara hiyo. Alisema samaki hao wachanga na wazazi waliovuliwa chini ya sentimita 30 na zaidi ya sentimita 85 wamekatishwa maisha yao.

Alisema takwimu za mavuno ya sangara waliokidhi kuvuliwa si chini ya sentimita 50 na sio zaidi ya sentimita 85 zinaonesha kushuka kutoka asilimia 19.9 (2005) hadi asilimia 6.1 (2015) “Mtu yeyote anayejihusisha na biashara ya samaki na mazao yake anatakiwa kupata leseni na vibali vya kununua na kusafirisha samaki, lakini kama unataka kufilisika jaribu kuingia kwenye shughuli za uvuvi haramu na miongoni mwa wale ambao Serikali imewapatia leseni kama watajiingiza kwenye uvuvi haramu, vibali na leseni zao zitafutwa,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwanaidi Mlolwa alisema samaki hao walikamatwa wakiwa wanakaushwa ambapo wamiliki wake walikimbia. Alisema Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya Mwaka 2003, Kifungu cha 37(a) (ii) na (iii) na kanuni zake za mwaka 2009, zinawapa mamlaka wasimamizi wa sheria kumkamata mtu yeyote anayekutwa na samaki na mazao yake waliovuliwa kwa njia haramu na kutaifisha mali zote ikiwemo samaki, boti, mitumbwi na magari yaliyobeba samaki hao. Mlolwa alisema licha ya wachakataji haramu hao kukimbia, watakamatwa kwa kuwa serikali ino mkono mrefu.