Walionusurika Lucky Vincent waanza kidato cha kwanza

WANAFUNZI watatu wa Shule ya Lucky Vincent walionusurika katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu Mei, 2017 kisha kupatiwa matibabu nchini Marekani, wameondoka mwishoni mwa wiki kwenda Shule ya Star High School iliyopo wilayani Arumeru kuanza masomo ya kitado cha kwanza.

Wanafunzi hao ambao ni Wilson Tarimo, Doreen Mshana na Sadia Awadh walionekana wenye furaha walipowasili katika shule yao ya Lucky Vincent na kukabidhiwa vyeti vyao vya kuhitimu elimu ya msingi na Mwalimu Mkuu Msaidizi, Longino Vincent.

Mtoto Wilson Tarimo alisema licha ya kuwa wote watatu walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya serikali, wanawashukuru wafadhili wao ambao ni Taasisi ya Siouxland Tanzania Educational Medical Ministries (STEMM) kwa kugharamia masomo yao.

Sadia Awadhi alisema anawashukuru watu wote waliwaombea wakati wakiwa kwenye matibabu na sasa wanaanza safari yao ya elimu ya sekondari wakiwa na afya njema na kuwasihi waendelee kuwaombea.

Mwenyekiti wa Bodi ya STEMM, Steve Meyer alisema kuwaona watoto hao watatu wakiwa na afya njema kwao ni muujiza mkubwa na kuahidi kuwa, wataendelea kuwagharamia mahitaji yao yote muhimu katika masomo.

Alisema Jiji la Sioux katika Jimbo la Iowa nchini Marekani limeahidi kuwa, iwapo watafanya vizuri katika masomo yao ya sekondari watapelekwa nchini humo kwa masomo ya chuo kikuu na wataendelea kushirikiana na Shule ya Lucky Vicent katika hatua zote.

Meyer alikabidhi Dola za Marekani 3,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 36.5 kwa ajili ya kusaidia elimu ya wanafunzi 14 wanaosoma katika Shule ya Lucky Vicent wasio na uwezo. Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Efraim Jackson alisema wazazi waliotambuliwa watoto wao watalipiwa nusu ada ya muhula mmoja ili kuwawezesha wapate elimu nzuri kulingana na mahitaji yao.