Kagame, Rubani wa Tanzania wang’ara tuzo ya Afrika

RAIS wa Rwanda, Paul Kagame na Mtanzania Suzan Mashibe ambaye ni rubani wa ndege za biashara na mhandisi, wametangazwa kuwa washindi wa Tuzo za Waafrika wa Mwaka 2017.

Katika tuzo hizo zinazotolewa na Jarida la Uongozi Afrika (ALM) la Uingereza, Rais Kagame amekuwa mshindi wa Tuzo ya Mwafrika wa mwaka 2017. Mashibe amepata tuzo ya Kiongozi Mwanamke Mwafrika.

Muethiopia Bethlehem Tilahum Alemu amepata tuzo kama hiyo. Mashibe ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tanjet Aviation inayotoa huduma katika usafiri wa anga nchini.

Mwaka 2009 alipata tuzo ya Wanawake Wenye Mafanikio, na mwaka 2011 Jukwaa la Uchumi la Dunia (WEF) lilimpa Mashibe Tuzo ya Kiongozi Kijana. Alemu ni mwanzilishi wa taasisi iitwayo SoleRebels ya nchini Ethiopia.

Rais Kagame, Mashibe na Alemu wamepata ushindi kwa kupata kura nyingi zilizopigwa kwa njia mbalimbali ikiwemo ya mtandao. Mchapishaji wa ALM, Dk Ken Giami amesema katika makao makuu ya jarida hilo kuwa, washindi hao watakabidhiwa tuzo zao Februari 24 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Rais Kagame ametwaa tuzo hiyo kwa kuwashinda marais wa nchi nne na wafanyabiashara wakubwa 12. Viongozi wengine waliowahi kupata tuzo ya Mwafrika wa Mwaka ni mwazilishi wa tuzo za uongozi za Ibrahim, Dk Mo Ibrahim (2010), na Rais Sirleaf (2011).

Wengine ni Rais wa zamani wa Nigeria Atiku Abubakar (2012), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha wa Mauritius, Xavier Luc-Duval (2013). Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne Tanzania, Jakaya Kikwete alishinda tuzo hiyo mwaka 2014, Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan (2015) na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mohammed Enterprise Tanzania Limited (MeTL), Mohammed `Mo’ Dewji (2016).

Tuzo za mwaka huu ni za sita, na zimetolewa katika vipengele saba. Strive Masayiwa wa Zimbabwe ameshinda Tuzo ya Afrika ya Maendeleo ya Elimu. Masayiwa ni mwanzilishi wa taasisi ya Econet.

Kwame Nana Bediako wa Ghana amepata Tuzo ya Uanzishaji Fursa za Ajira. Bediako ni Rais, mwanzilishi, na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Petronia Ghana. Rais wa zamani wa Madagascar, Marc Ravalomanana amepata Tuzo ya Uongozi kwenye Siasa.

Mwenyekiti wa Comcraft Group, Kenya, Manu Chandaria ameshinda tuzo ya Upendo na Michango ya Hiyari kwa Jamii. Joel Macharia amepata Tuzo ya Kijana wa mwaka 2017. Kijana huyo ni mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Abacus Kenya