Aliyetolewa kifungoni na JPM aliza waumini kanisani

MMOJA wa wafungwa waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na kutoka kwa msamaha wa Rais, Desemba 9, mwaka jana, Raphael Mlyuka amewatoa machozi waumini walioshiriki ibada yake ya shukrani, baada ya kueleza machungu aliyoyapitia wakati akitumikia kifungo chake.

Katika hatua nyingi, Mlyuka ameliambia gazeti hili katika mahojiano maalumu kuwa amemuandikia barua rasmi Rais John Magufuli kumshukuru kwa msamaha huo. Alisema barua hiyo imepitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri na kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka.

Mlyuka aliwatoa machozi waumini walioshiriki ibada ya kutoa shukrani ya pekee ya kumshukuru Mungu kwa kumtoa gerezani, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Njombe. Alisema anamshukuru Rais Magufuli na serikali kwa jumla kwa kuamua kumfutia adhabu ya kukaa jela maisha.

Alisema pia anamshukuru Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere kwa kumbadilishia adhabu kutoka kifo kuwa kifungo cha maisha Desemba 10, 1982, hatua iliyosababisha kupata msamaha wa Rais Magufuli. Akizungumza huku akitoa machozi ya furaha mbele ya ndugu, jamaa na marafiki, hali iliyowafanya ndugu na marafiki zake nao kuanza kulia, Mlyuka alisema ingawa, hakutenda kosa la mauaji lililomsababishia aende jela, anamshukuru Mungu.

“Ninakiri mbele yenu ndugu zangu na mbele ya Mungu wangu ambaye anaona sirini, sikushiriki katika mauaji yale yaliyonifanya nikae jela miaka 43 na endapo ningenyongwa ningekuwa nimeonewa kwa kuwa sijui chochote kuhusu mauaji yale,” alisema Mlyuka. Akizungumza kuhusu afya yake, alisema ana matatizo ya miguu, mgongo, fangasi, kisukari na shinikizo la damu, hali inayomfanya ashindwe kutembea mwenyewe bila msaada wa mtu mwingine.

Mlyuka alisema alifungwa akiwa na umri wa miaka 34 akiwa na wake watatu na watoto 10, lakini amerudi na kukuta wake zake wawili, mama na baba yake mzazi, dada yake na watoto wake wanne wamefariki dunia huku akiwa na wajukuu 22 na vitukuu sita. Alisema alianza kutoa shukrani ya pekee kwa Mungu, Desemba 31, mwaka jana kijijini kwao alikozaliwa Nyenyembe, Kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi mkoani Iringa, lakini aliona haitoshi hivyo ni bora kumshukuru Mungu katika eneo ambalo alikuwa anaishi awali; Njombe mjini.

Akizungumza na waumini baada ya kupokea sadaka hiyo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Njombe, Isaya Mengele aliwataka Watanzania kuendelea kumuombea Rais Magufuli na kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii. Baadaye katika mahojiano maalumu na HabariLeo nyumbani kwake, Mtaa wa Mahakama ya Mwanzo, Kitongoji cha Gwivaha, Kata ya Njombe Mjini jana, Mlyuka alisema tayari amemuandikia barua rasmi Rais Magufuli ili kumshukuru kwa msamaha huo.

Alisema alitamani kwenda Ikulu kumshukuru ana kwa ana, lakini anatambua kuwa ana majukumu mengi ya kitaifa, na pia afya na hali yake (Mlyuka) kiuchumi si nzuri na kwamba, ndiyo maana ameamua kutumia barua. Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri, aliahidi kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa kuifikisha barua hiyo kwa Rais Magufuli kwa wakati mwafaka.

Wakizungumza na Habari- Leo, majirani wa Mlyuka Maria Chale na Lucia Mapunda, walimshukuru Rais Magufuli na kumuombea Mungu ampe maisha marefu na kumlipa kwa wema aliyoutenda kwa ndugu yao. Walisema adhabu ya Mlyuka iliwaumiza kwa kuwa alikuwa ni kijana mzuri ambaye hakuwa na sifa zozote za wizi hivyo kitendo kile kilizua taharuki kubwa kwa ndugu jamaa na marafiki.

Mjukuu wa Mlyuka; Suzan Kinyunyu akiwa na furaha alisema hakuwa anamfahamu babu yake kwa kuwa alizaliwa wakati yupo jela, bali alikuwa akisimuliwa na mjomba wake kuhusu babu yake hali aliyosema ilikuwa ikumuumiza. Alisema waliendelea na sala za kumuomba Mungu angalau siku moja babu yao atoke akiwa mzima na Mungu alisikia maombi yao hatimaye, ametoka. Alisema wanashukuru pia Rais Magufuli kwa msamaha huo kwa babu yao ambao hawakuutarajia.