JPM apokea taarifa za Airtel, Madini

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha taarifa ya kamati aliyoiunda kuchunguza umiliki wa Kampuni ya Simu ya Airtel kwa Rais John Magufuli, aliyeagiza kufanyika kwa uchunguzi huo Desemba 20, mwaka jana.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amekamilisha Kanuni za Sheria ya Madini Namba 7 ya mwaka 2017 na kuwasilisha vitabu vya kanuni hizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

Taarifa nyingine iliyowasilishwa kwa Rais ni ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Novemba 25, mwaka jana wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Akiwasilisha taarifa yake, Dk Mpango alisema Serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel, ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu. Kufuatia ukiukwaji huo, Dk Mpango alisema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni ya Airtel, imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.

“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya, lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao,” alisema Dk Mpango.

Wakati huo huo, Rais Magufuli jana alipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Novemba 25, mwaka jana wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Baadhi ya maagizo hayo ni kupunguza baadhi ya idara na madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhamishia Mloganzila na hospitali za mikoa kuhamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Waziri Ummy aliwasilisha taarifa hiyo, akiwa ameongozana na viongozi wakuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (MUHAS).

Kwa upande wake, Profesa Kabudi akiwa na Naibu Mawaziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Doto Biteko, alisema Kanuni hizo zimekamilika siku moja kabla ya tarehe ya mwisho, iliyotolewa na Rais Magufuli na kubainisha kuwa sasa sheria inaweza kuanza kutumika. Kwa upande wao, naibu mawaziri wa nishati waliwataka Watanzania na wadau wote wa sekta ya madini, kushirikiana na Serikali kutekeleza sheria hiyo na wamempongeza Rais Magufuli kwa kutoa msukumo wa kukamilishwa kwa kanuni hizo.