Mbunge barazani kwa deni la mil 12/-

MBUNGE wa Kilwa Kusini kupitia Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Lindi, Selemani Bungara maarufu Bwege, amefi kishwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Lindi kwa kutuhumiwa kutolipa deni la Sh milioni 12 analodaiwa na Hamisi Kaudunde tangu Februari 28, 2016.

Deni hilo limetokana kwa kuuziana viwanja saba vyenye thamani ya Sh milioni 42, ambazo kati ya hizo, Sh milioni 30 zilishalipwa tangu mwaka juzi. Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Lindi, Said Wambili alisema kwamba kesi hiyo namba 50 ya mwaka 2017, imefunguliwa Oktoba mwaka jana.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba kwa mkataba waliokubaliana baina yao, Kaudunde na Bungara, mbunge huyo alitakiwa ifikapo Februari 28, 2016 kiasi kilichosalia Sh milioni 12 kiwe kilishalipwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi alitaja viwanja hivyo kuwa viko katika barabara ya Nangurukuru Kilwa Masoko. Namba za viwanja hivyo ni 17(A), 18 (A), 19(A), 19(1A), 22(A), 23(A) na 24(A), vyote vina thamani Sh milioni 42.

Naye Bungara alithibitisha kununua viwanja hivyo kwa fedha hizo na alilipa Sh milioni 30 na kubakia deni la Sh milioni 12. Alisema alisita kumalizia deni hilo baada ya kubaini kuwa viwanja hivyo havikupimwa.