CCM yanyakua Singida Kaskazini, Songea Mjini

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepata ushindi wa kishindo katika majimbo ya Singida Kaskazini Mkoani Singida na Songea Mjini mkoani Ruvuma. Wagombea wa chama hicho Justine Monko Joseph wa Singida Kaskazini katangazwa leo kuwa mshindi kwa kura zaidi ya 20,000 kati ya 22,000 zilizopigwa.

Kwa upande wa Songea Mjini, mgombea wa CCM, Damas Ndumbaro amepata ushindi kwa kura 45,162 na kumuacha mgombea wa CUF aliyepata kura 608. Uchaguzi huo mdogo wa ubunge katika majimbo ya Longido mkoani Arusha, Songea Mjini mkoani Ruvuma na Singida Kaskazini (Singida), ulifanyika jana kwa amani.

Katika Jimbo la Longido, ulifanyika kwa amani na utulivu mkubwa huku baadhi ya watu wakimiminika katika vituo vya kupiga kura kutimiza demokrasia yao ya kumchagua mbunge wa jimbo hilo.

Uchaguzi huo unarudiwa kufanyika baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutengua ubunge wa Mbunge wa Chadema, Onesmo ole Nangole kutokana na ukiukwaji wa sheria ya uchaguzi katika ushindi wake.

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Stephen Kiruswa alipiga kura katika Kituo cha Ngosuk Shuleni kilichopo katika Kata ya Engarenaibor kutimiza wajibu wake wa kupiga kura.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa uchaguzi katika jimbo hilo, Juma Mhina alisema vifaa vyote na wasimamizi wa uchaguzi huo walifika salama katika vituo vya kupiga kura na jimbo hilo lina jumla ya vituo 175 na vituo hivyo vilifunguliwa saa 1.30 asubuhi.

Alisema uchaguzi huo unahusisha vyama tisa vya siasa, lakini juhudi za kuwapata wagombea hao kujua maeneo waliyopiga kura zilikuwa ngumu kwani ilielezwa walijiandikisha katika kata zilizo mbali na makao makuu ya jimbo.

Mhina aliwataja wagombea ubunge waliojitokeza kuwania ubunge katika jimbo hilo ni pamoja na mgombea wa CCM, Dk Kiruswa, Kisiyongo Ole Kurya (CUF), Francis Ringo (CCK), Feruzily Feruzilyson (NRA), Simon Ngilisho (CDM), Godwin Sarakikya (TADEA), Simon Bayo (SAU), Mgina Mustafa (AFP) na Robert Laizer (TLP).

Alisema Longido ina kata 18 na vituo 175 vya kupiga kura na waliojiandikisha kupiga kura ni wananchi 57,808. Hadi tunakwenda mitamboni hakukuwa na vurugu zozote katika uchaguzi huo na vituo vilifungwa saa 10:00 kamili kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wananchi walikuwa wakisubiri ujumlishwaji wa kura kutoka katika kata zote 18 kuletwa katika majumuisho makao makuu ya halmashauri.

Kwa mujibu wa taarifa za vituo 11 vya kupiga kura katika Jimbo la Jimbo la Longido, mgombea wa CCM, Dk Kiruswa alikuwa akiongoza na kuwaacha kwa mbali wagombea wenzake wanane. Kati ya vituo hivyo vya kupiga kura ambavyo matokeo yake yamebandikwa nje kwenye ubao wa matangazo, Dk Kiruswa alikuwa akiongoza kwa kura 5,675.

Taarifa hiyo inaonesha wagombea wa vyama nane vya upinzani jumla walikuwa na kura 77 katika vituo hivyo. Katika majimbo ya Singida Kaskazini na Songea Mjini pia wananchi walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo ambao chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hakijashiriki.

Katika uchaguzi huo, jumla ya vituo 742 vya ubunge vitahusika kupigia kura, huku kukifanyika pia uchaguzi katika kata tano zenye vituo 856. Jimbo la Singida Kaskazini limefanya uchaguzi huo kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wake, Lazaro Nyalandu aliyefukuzwa uanachama wa CCM mwishoni mwa mwaka jana kisha kujiunga na Chadema.

Jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma liko wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge, Leonidas Gama. Aidha, kata tano zilizohusika katika uchaguzi wa madiwani ni Keza iliyoko Halmashauri ya Ngara, Kimandolu ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, Kurui ya Kisarawe, Bukumbi ya Tabora Uyui, na Kwagunda wilayani Korogwe.

Kata ya Kihesa iliyopo Iringa, mgombea wake amepita bila kupingwa, hivyo haitoshiriki katika uchaguzi huo. Katika uchaguzi huo mdogo, vyama vilivyojiorodhesha kushiriki ni Ada Tadea, AFP, CCM, Demokrasia Makini, NRA, Sauti ya Umma (SAU), TLP, Chama cha Wananchi (CUF), CCK, DP, na UPDP.