Hali ilikolipuka gesi Buguruni sasa shwar

HALI sasa ni shwari kwenye mtaa wa Mjimpya Kata ya Buguruni kwa Mnyamani, Ilala Dar es Salaam ambako bomba la gesi lililipuka karibuni.

Mlipuko huo ulisababishwa na kupasuka kwa bomba la gesi wakati wafanyakazi wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) wakichimba mitaro kusambaza mabomba ya maji mlipuko wa moto ukatokea.

Gazeti hili lilitembelea eneo hilo juzi na jana kutathmini hali ilivyo kuanzia kona ya Buguruni kwa Mnyamani hadi mwisho wa barabara hiyo eneo la Vingunguti likishuhudia mambo kadhaa.

Katika eneo la Mjimpya lilikolipuka bomba hilo, Mwanaisha Hassan anayeishi mtaa huo alisema awali bomba lilipolipuka hali ilikuwa tete hadi siku mbili lilipokuja kutengenezwa. Alisema bomba hilo sasa limefukiwa kabisa na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Rahma Sufiges amesema kwa sasa hakuna tena tatizo.

Wafanyabiashara waliokuwa wakiuza bidhaa za vyakula eneo lililolipuka walionekana kufanya biashara kwa mbali kukiwa na bomoabomoa iliyoanzia mabanda ya Ilala hadi Pugu ikihusisha mabanda ya mitumba na vyakula.

Katika eneo la njia za Buguruni kwa Mnyamani mwandishi alishuhudia maduka na magenge yamefungwa kufuatia kufungwa kwa barabara ianziayo Vingunguti hadi Shell kwa Mnyamani.

Akizungumzia kufungwa kwa biashara hiyo na athari zake kwa biashara, Juma Ramadhani mkazi wa eneo hilo anayeuza duka la nguo alieleza imeathiri biashara nyingi licha ya kuwa matengenezo yanayofanyika ni muhimu pia.

Utandazwaji wa mabomba hayo ulitarajiwa kumalizika jana kwa kuwa ulipangwa kufanyika kwa siku 14 kuanzia Januari 5 mwaka huu na kusimama kwa muda kutokana na mlipuko huo.