‘Wauaji wanaokimbilia Msumbiji kukiona’

WAKUU wa Polisi wa Tanzania na Msumbiji, wamesema wahalifu wakiwamo waliofanya mauaji nchini Tanzania na kukimbilia nchi jirani ya Msumbiji, hawako salama, kwa kuwa wanashughulikiwa na vyombo vya usalama.

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) wa Tanzania, Simon Sirro (pichani) na IGP wa Msumbiji, Bernadinho Rafael, walisema hayo jana wakati wakitia saini makubaliano ya kushirikiana kudhibiti uhalifu na kubadilishana taarifa kuhusu wahalifu wanaovuka mipaka baina ya nchi hizi.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam jana, IGP Sirro alisema; “Tunatia saini makubaliano ya kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu Tanzania na Msumbiji katika kukabili matishio ya ugaidi, dawa za kulevya na makosa ya kuvuka mipaka ili tufanye kazi pamoja katika operesheni mbalimbali kwa kubadilishana taarifa ili Watanzania na watu wa Msumbiji waishi kwa amani.”

Sirro alisema hata wahalifu waliofanya mauaji katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na kwingine kisha kukimbilia Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) au nchi nyingine, hawako salama maana kwa umoja uliopo, mtu akifanya uhalifu akakimbilia DRC, Msumbiji, au Rwanda, hatakuwa salama.

“Ukijiingiza katika makosa ya kutumia silaha, utapata majibu yake kupitia silaha, hivyo dawa ni kuacha uhalifu na mambo ya hovyo,” alisema IGP Sirro na kuongeza, “Tunashirikiana kudhibiti uhalifu ili Afrika Mashariki iwe salama, na watu wa Msumbiji na Tanzania waishi kwa utulivu.”

Naye IGP Rafael wa Msumbiji alisema, “Tumeamua kushirikiana kwa dhati kupambana na uhalifu katika nchi hizi likiwamo tishio la ugaidi na makosa mengine yanayohatarisha usalama wa watu katika nchi hizi.”

Mkuu wa Polisi huyo wa Msumbiji alisema wamefikia hatua hiyo kwa kuwa ni wazi penye uhalifu hakuna maendeleo tarajiwa. Alisema ushirikiano huo umemlenga kudhibiti wahalifu na uhalifu wa aina mbalimbali yakiwamo mauaji yanayofanywa dhidi ya wananchi na watu wenye ualbino sambamba na kukabili uhamiaji haramu.