Wapitisha Muswada kubana ukatili kwa wanandoa

BUNGE la Rwanda limepitisha muswada wa mabadiliko ya sheria inayotoa adhabu ya kifungo cha miaka 10 hadi 15 kwa mwanandoa anayepatikana na hatia ya kubaka wenza wao.

Rais Paul Kagame anasubiriwa kusaini mabadiliko hayo ili sheria hiyo ianze kutumika. Kwa mujibu wa hukumu ya sheria inayotumika sasa inayobainishwa kwenye Kanuni za Adhabu, anayepatikana na hatia ya kumbaka mtu mwenye umri wa miaka 18 na zaidi anafungwa jela zaidi ya miaka mitano hadi saba.

Kwa sheria inayotumika sasa mwanandoa anayepatikana na hatia ya kumbaka mwenzi wake anahukumiwa kifungo jela kuanzia miezi miwili na si zaidi ya miezi sita. Kifungu cha 133 cha muswada uliopitisha kinabainisha kuwa, mtu anayepatikana na hatia ya kubaka anastahili kifungo jela kisichopungua miaka 10 na kisichozidi miaka 15.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, anayepatikana na hatia hiyo pia atatozwa faini isiyopungua Faranga milioni moja za Rwanda na zisizozidi Faranga milioni mbili za nchi hiyo. Kifungu hicho kinabainisha pia kwamba, kitendo cha kubaka kikifanywa miongoni wa wanandoa pia itatambulika kuwa ni kubaka hivyo kutokuwa tofauti na ubakaji mwingine.

Wakati wa kuujali muswada huo, Mbunge Theoneste Karenzi alisema “Kubaka ni kubaka bila kujali uhusiano na uadhibiwe kwa hivyo”. Alisema, kama mwanandoa anambaka mwenza wake ina maana kuna tatizo kubwa na liadhibiwe vikali. “Kama mtu anakwenda kulalamika kuhusu kubakwa na mwenza wake ina maana kwamba, tatizo ni kubwa zaidi,” alisema.