Majaliwa asitisha ujenzi wa ofisi ya halmashauri

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesitisha uamuzi wa ujenzi wa makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Tarime katika eneo la Nyamwaga baada ya kubaini kutaifanya halmashauri hiyo itumie fedha nyingi kwa ajili ya ulipaji fi dia wakazi wa maeneo hayo.

Alitangaza uamuzi huo mjini Tarime mkoani Mara alipozungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri ya wilaya na mji wa Tarime. Alisema haina haja ya kutumia pesa nyingi kwa kitu kinachoweza kuepukika huku kukiwa na maeneo yanayoweza kutumika bila kulipa fidia.

Alisema mbali na fedha nyingi za fidia ya eneo hilo, lakini pia uteuzi wake haukufuata taratibu na haukuzingatia jiografia ya halmashauri hiyo katika kuwasogezea wananchi huduma muhimu. Alisema baada ya kufanya uamuzi huo, serikali itatuma wataalamu Tarime Vijijini ili kuangalia maeneo hayo kisha kutoa ushauri wa eneo lipi linastahili kujengwa makao makuu hayo.