Polisi wakanusha kukamata wanaovaa vimini

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekanusha kuwepo kwa operesheni ya kuwakamata watu wanaovaa nguo fupi maarufu kama ‘vimini’ na milegezo katika mkoa huo.

Limesema operesheni yake ni ya kukamata watu wanaovaa nguo fupi na kina dada wanaofanya biashara ya ukahaba kwa kuwa hao wanatenda kosa kinyume cha sheria ya nchi. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alikuwa akifafanua taarifa iliyoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa kuna operesheni ya kukamata wanaovaa nguo fupi.

Alisema juzi alikuwa na mkutano na waandishi wa habari na kulikuwa na swali kuhusu ukamataji wa watu wanaovaa nguo fupi ambapo alisema hakuna msako wa namna hiyo badala yake, alisema, Polisi wanakamata watu wanaofanya vitendo vinavyovunja sheria iliyotungwa na mamlaka zilizopewa dhamana na siyo kuwakamata wanaovaa nguo fupi.

Alisema alichokieleza juzi ni kuwa inategemea ni wapi ulipovalia nguo hizo na kueleza kwa mfano eneo la fukweni ’beach’ ambalo ni eneo watu kustarehe hawategemei mtu aende na makoti mazito na suti katika maeneo hayo kwa kuwa kuna nguo zake rasmi za kuogelea huko.

Alisema nguo fupi inategemea inavaliwa wapi na watashangaa mtu atakayevaa nguo fupi akakutwa kanisani au mahali penye staha. “Sikueleza kama kuna msako watu wanaovaa nguo fupi isipokuwa nilichokisema ni kwamba kuna matendo mtu anaweza kuyafanya ambayo ni kinyume cha maadili ya Mtanzania. Watanzania wana utamaduni wao wa mavazi, mavazi mafupi ni kuiga tamaduni za wageni ambapo kwao hata wakija huku wanakuwa na nguo zinazokubalika mataifa yao,”alisema.