Waziri: Bajeti ununuzi wa dawa Zanzibar imeongezwa

WIZARA ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imejipanga kuhakikisha bajeti ya wizara hiyo inaimarishwa kwa ajili ya kuweza kutoa huduma ikiwemo za ununuzi wa dawa.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo wakati akizungumza na wafanyakazi wa hospitali ya Chake Chake akiwapa taarifa juu ya nia ya serikali chini ya Rais Ali Mohamed Shein katika kuimarisha sekta hiyo. Alisema Serikali imejipanga vizuri kuongeza bajeti ya sekta hiyo ikiwemo ununuzi wa dawa muhimu za binaadamu ambapo katika mwaka wa fedha wa 2016/17 zilitengwa jumla ya Sh bilioni 4.9 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.

Aidha, alisema katika mwaka wa bajeti 2017/18, Serikali ilitenga jumla ya Sh bilioni saba kwa ajili ya ununuzi wa dawa katika hospitali zake zilizopo Unguja na Pemba. Aliongeza kuwa mwaka 2018/19, bajeti ya ununuzi wa dawa muhimu za binadamu utaongezwa na kufikia Sh bilioni 12. “Hiyo ndiyo sehemu ya mikakati yetu katika kuimarisha huduma za afya na ununuzi wa dawa muhimu za binadamu, tunaelekea katika kutoa matibabu bure,” alisema.

Aliyataja mafanikio yaliyopatikana kwa sasa ni kwamba hakuna mtu anayetembea kilomita mbili kwa ajili ya kutafuta huduma za afya ikiwemo vijijini. Aidha huduma za wajawazito zimeimarika kuanzia mjini hadi vijijini kiasi ya kuyafikia malengo ya dunia endelevu katika huduma bora za akinamama na watoto. Matarajio yetu kuyafikia malengo endelevu ya dunia huku tukipunguza ugonjwa wa Ukimwi na kufikia asilimia 0.4 pamoja na malaria ambayo ipo kiwango hicho cha 0.4 katika mwaka 2017.