Chadema yateua wagombea ubunge Kinondoni, Siha

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeamua kurudi ‘uwanjani’ katika uchaguzi wa ubunge baada ya kususia ule wa hivi karibuni kwa kutangaza kushiriki na kutaja majina ya wagombea katika Uchaguzi Mdogo utakaofanyika Februari 17, mwaka huu.

Chadema ilikataa kushiriki Uchaguzi Mdogo wa majimbo ya Singida Kaskazini (Singida), Longido (Arusha) na Songea Mjini (Ruvuma) pamoja na kata sita nchini, hivi karibuni kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.

Lakini jana chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania Bara, kilitangaza majina ya wanachama wake waliopitishwa kugombea ubunge katika majimbo ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 17, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, waliopitishwa kugombea ubunge ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu atakayegombea Jimbo la Kinondoni na Elvis Mosi aliyeteuliwa kugombea Jimbo la Siha.

Mrema alisema wagombea wote wameshachukua fomu za uteuzi kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi kwenye majimbo husika na watazirejesha leo kwa ajili ya uteuzi utakaofanyika Januari 20, kabla ya kuanza kwa kampeni za vyama vyote Januari 21 hadi Februari 16, ili vinadi sera zao kuelekea katika uchaguzi huo.

“Kamati Kuu ya Chama imemaliza vikao vyake leo (jana) na imefanya uamuzi wa kushiriki kwenye Uchaguzi Mdogo kwenye majimbo ya Kinondoni na Siha unaotarajiwa kufanyika Februari 17,” ilisema taarifa ya Mrema.

Majimbo hayo mawili yanarudia uchaguzi baada ya waliokuwa wanayashikilia, Maulid Mtulia (Kinondoni –CUF) na Dk Godwin Mollel (Siha – Chadema) kujiuzulu nafasi zao kwa nyakati tofauti na kuhamia CCM mwezi uliopita kwa madai ya kutaka kumuunga mkono Rais John Magufuli.

Tayari Mtulia na Dk Mollel waliojiunga na CCM, wameshapitishwa na chama hicho tawala kuwania tena nafasi hizo na tayari wamechukua fomu kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi ili kupitishwa ‘kutetea’ nafasi hizo