CCM, Chadema na CUF watambiana Kinondoni

WAGOMBEA wa vyama mbalimbali wanaowania nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kinondoni, wamerudisha fomu, huku mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Maulid Mtulia akiahidi kufanya kampeni za kistaarabu.

Wagombea hao walirudisha fomu hizo kwa nyakati tofauti kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.

Mtulia alisema, “Nashukuru chama changu kwa kuniamini na kuniteua kugombea katika Jimbo la Kinondoni, nawashukuru pia wanachama wenzangu wa CCM kwa kuupokea uamuzi wa Kamati Kuu ya chama”.

Alisema amekamilisha fomu na kampeni wanatarajia kuzianza leo, na kuahidi kwamba watafanya kampeni za kistaarabu kama kawaida ya chama hicho. “Nawaomba vyama vingine tufanye kampeni za kistaarabu, kwa kuwa Kinondoni ndiyo Dar es Salaam na kwa kuwa Dar es Salaam ndiyo Tanzania hivyo Kinondoni ni Tanzania na lazima tuwafundishe wengine kampeni za kistaarabu na demokrasia ikoje, hatutawaangusha wanaCCM,” alisema Mtulia.

Mbunge huyo wa zamani wa CUF alijiuzulu wadhifa huo hivi karibuni na kuhamia chama tawala na ndiyo sababu ya kuwapo kwa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kinondoni. Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifwamba alisema wamefuata taratibu zote, na uchaguzi huo ni wa mkoa hivyo watashiriki viongozi wote wa chama wa mkoa huo kuanzia shina hadi mkoa na umoja na mshikamano ndiyo silaha ya ushindi wao.

“Tumejipanga tutapata ushindi wa kihistoria kwa kuwa sisi hatuna zawadi ya kumpa Mwenyekiti wetu wa chama kwa kazi nzuri anayofanya ya kuimarisha chama na umoja na mshikamano kwa Watanzania, hivyo ushindi wa Kinondoni ni zawadi yetu kwake,” alisema Mwakifwamba.

Aliwataka wanaCCM kujitokeza kwa wingi kufanya kampeni za kistaarabu kwa sababu wao ni walimu wa ustaarabu na wenzao watajifunza kutoka kwetu. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Harold Maruma alisema wanaelekea kuchukua jimbo hilo ‘mchana kweupe’ na kuwataka wapinzani kufanya kampeni za kistaarabu badala ya za kihuni kwa kuwa wamejipanga.

Kwa upande wake, mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Rajab Juma aliwataka wananchi kutovunjika moyo na kukichagua chama hicho kwani bado kimejipanga kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha, alikituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kudhoofisha upinzani kwa kumsimamisha mgombea wakati jimbo hilo kimkakati lilikuwa ni la CUF.

“Kama walishindwa kuweka mgombea katika jimbo lililokuwa na mgombea wao kwa madai kwamba kuna mapungufu inakuwaje sasa wameweka mgombea kwenye jimbo hili ambalo tayari CUF imesimamisha mgombea?

Hii inaonesha wazi kwamba hawana dhamira ya kukuza demokrasia hapa nchini,” alisema. Akijibu tuhuma hizo, mgombea wa Chadema, Salim Mwalimu alisema wanachosubiri ni busara za wananchi ndiyo wenye kujua hatma ya Jimbo la Kinondoni.

Aliahidi kwamba leo jioni watazungumza na waandishi wa habari na kuelezea ratiba ya kampeni. Aliwashauri wananchi wa Kinondoni na wanachama wa Chadema kwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza kurudisha fomu hiyo na kuwaomba kushiriki kwa wingi zaidi huku akisisitiza kwamba wamejipanga, hawabipu bali wanamaanisha.

“Kama ni nidhamu ya siasa waliyoikataa naamini Kinondoni watairudisha na wasipoirudisha maana yake ustaarabu katika siasa utakuwa umemalizika... Hatutakuwa wa kulia tena, bali ikibidi wale waliotufanya tulie watalia wao.

Nimedhamiria kuitafuta haki ya watu wa Kinondoni sitoyumba,” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema Zanzibar ambaye alishindwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 katika Jimbo la Kikwajuni.

Aliongeza kuwa, “Nitafanya kampeni zenye kuleta umoja na mshikamano kwa wananchi wa Kinondoni bila kujali tofauti zetu za vipato, imani na kiitikadi, nitakwenda kuwaunganisha katika kupigania haki, demokrasia, maendeleo na maslahi yetu wananchi wa Kinondoni”.