Bandari Dar sasa kumekucha

BANDARI ya Dar es Salaam imeongeza ufanisi kwa kupakua magari zaidi ya 600 kwa siku yakiwa tayari kukabidhiwa kwa wateja, kutoka wastani magari 150 kwa mwaka mmoja uliopita.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Freddy Liundi, alisema ufanisi huo upo pia katika mizigo mingine, yakiwemo makasha.

Liundi alisema kwa sasa bandari yao inafanya vizuri, kuanzia upakuaji na utoaji wa makasha pamoja na magari kulinganisha na hali ya utendaji ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. “Mwaka mmoja tu uliopita, Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa inatoa magari 100 mpaka 150 tu kwa siku, lakini tumejipanga upya, tumetoa elimu kwa wafanyakazi wa kitengo cha magari, sasa tuna uwezo wa kutoa magari, kwa maana ya kuwapa wateja, zaidi ya gari 600 kwa siku.

“Hivyo kuna mabadiliko makubwa yametokea katika bandari ya Dar es Salaam na tunaendelea kusimamia ufanisi zaidi,” alisema Liundi. Alisema kuongeza ufanisi maradufu katika bandari ya Dar es Salaam, usalama wa mizigo na gharama nafuu anazopata mteja, vimevutia wateja wengi kutoka nchi jirani kutumia bandari hiyo kulinganisha na bandari nyingine shindani.

Alisema wanajitahidi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, lakini wakati mwingine matatizo yanayotokea husababishwa na wadau wao wanaoshirikiana nao kupokea na kusafirisha mizigo.

Alisema matatizo pia huweza kusababishwa na wateja wenyewe kwa kutokamilisha taratibu za kiforodha zinazotakiwa ili kutoa mzigo haraka. Baadhi ya wadau wanaoshirikiana na TPA kwa kila mzigo unaopitia bandarini ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Bandari Kavu (ICDs) na mawakala waliosajiliwa kwa ajili ya kusaidia wateja kutuma na kutoa mizigo bandarini.

Mahojiano kamili ya viongozi wa TPA akiwemo Liundi yatakuwa yakichapishwa kila Jumanne katika gazeti hili. Hii ni nafasi yako msomaji kujua shughuli mbalimbali za bandari na unavyoweza kufaidika nayo kibiashara.