EAC yajiimarisha viwanda vya magari

GARI la kwanza lililotengenezwa Rwanda, linatarajiwa kuwa barabarani Mei mwaka huu, imefahamika. Kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen (VW) ya Ujerumani, ipo kwenye maandalizi ya kutengeneza aina tatu za magari nchini humo.

VW imetangaza kuwekeza Dola za Marekani milioni 20 (takribani Faranga bilioni 17 za Rwanda) kwenye uanzishaji kiwanda cha kutengeneza magari nchini humo. Uongozi wa kampuni hiyo umesema sehemu kubwa ya fedha hizo, zitatumika kutengeneza magari na kuanzisha maeneo ya uunganishaji magari.

Kampuni hiyo tayari imesajili kampuni nchini humo iitwayo, Volkswagen Mobility Solutions Rwanda. Wakili Athanase Rutabingwa ni Mkurugenzi Mkazi wa kampuni hiyo. Ofisa Mtendaji Mkuu wa VW nchini Afrika Kusini, Thomas Schafer alisema, wamechagua kuwekeza Rwanda kwa kuwa kuna mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Schafer pia ni mwakilishi wa VW barani Afrika. “Tulichagua Rwanda kwa sababu kuna utulivu wa kisiasa, wanapambana na rushwa, ukuaji asilimia saba (uchumi), idadi ya watu vijana na yenye ufahamu wa teknolojia.

VW inapata msaada mkubwa kutoka Serikali ya Rwanda na ushirikiano kutoka Bodi ya Maendeleo Rwanda unaongoza ajenda ya Smart City,” alisema Schaefer. Kutengenezwa magari Rwanda ni matokeo ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya Serikali ya nchi hiyo na Volkswagen Desemba mwaka 2016.

Pande hizo mbili zilifanya upembuzi yakinifu Septemba mwaka jana na kuridhika kuwa uwekezaji huo utakuwa na manufaa. “Kenya tunatengeneza Polo Viva na hapa tunatengeneza aina tofauti. Hata kama tunaanzisha kitu fulani kipya Kenya, kitakuwa tofauti na kinachotengenezwa Rwanda,” amesema Schaefer.

Kiwanda cha Rwanda kinatarajiwa kujengwa kwenye eneo la Ukanda Maalumu wa Kiuchumi (SEZ) na kitakuwa na uwezo wa kutengeneza magari 5,000 kwa mwaka. Kwenye eneo la hilo, pia kutakuwa na duka la kuuza magari na eneo la matengenezo.

Kwenye awamu ya kwanza, kiwanda cha Rwanda kinatarajiwa kuajiri watu kati ya 500 hadi 1,000. Schafer alisema kiwanda hicho kinaweza kuanza kazi kabla ya mwisho wa Mei mwaka huu.

“Tunajaribu kuondoa huu mtazamo kwamba, Afrika ni masikini; hawawezi kumudu kununua magari,” alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Kigali. Kwa kuanzia kiwanda cha Rwanda kitatengeneza magari madogo ya kutembelea aina ya Volkswagen Passat, Volkwagen Polo na Volkswagen Teramont.

VW itatengeneza magari nchini humo kwa kuzingatia mtazamo uitwao ‘ThinkBlue cars’. Mtazamo huo unahusu magari rahisi kuyahudumia, na rafiki wa mazingira kwa kuwa yanatumia mafuta kidogo na kutoa moshi kidogo.

Schafer alisema awamu ya kwanza ya VW kwenye uchumi wa Rwanda kwa kiasi kikubwa, itahusisha ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha magari na mafunzo. Uwekezaji wa VW Rwanda utafanywa kwa awamu tatu.

Kwa mujibu wa Schafer, baadhi ya mitambo itakayotumika kwenye kiwanda hicho ipo njiani kupelekwa bandari ya Mombasa na kwamba kazi zitaanza haraka kadri itakavyowezekana.

VW wanasema wamevutiwa na ukuaji wa soko la Rwanda na wana malengo ya muda mrefu kuwekeza nchini humo. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo Rwanda (RDB), Clare Akamanzi, ameikaribisha VW kwenye soko la Rwanda na anaamini uwekezaji huo utawanufaisha vijana nchini humo.

“Tumefurahi kufungua huu ukurasa mpya kama nchi. Tangazo hili ni ushahidi wa maendeleo yaliyopatikana tangu tuliposaini MOU mwaka 2016.Tuna uhakika kwamba, ushirikiano na VW utatengeneza fursa nyingi kwa Wanyarwanda vijana,” alisema Akamanzi kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Akamanzi, mwaka jana kulikuwa na magari 300,000 kwenye nchi hiyo yenye watu milioni 12. Amesema, uwekezaji wa Volkswagen nchini humo ni nyongeza katika ongezeko la uwekezaji kutoka nje ya nchi hiyo.

“Katika miaka 10 iliyopita, uwekezaji ulioandikishwa Rwanda umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 kutoka Dola za Marekani milioni 800 mwaka 2007 hadi Dola bilioni 1.675 za Marekani mwaka 2017.

Huu ni uthibitisho kwamba Rwanda inaonekana eneo lenye mvuto kwa uwekezaji” alisema Akamanzi. MAGARI YA TANZANIA Wakati hayo yakiendelea nchini Rwanda, Tanzania nayo inazidi kufanya vizuri kwenye ubunifu na sasa inatengeneza na kuuza nje magari ya kubeba watalii na malori ya takataka.

Kampuni ya Hanspaul Automechs Limited (HAL) iliyopo kwenye eneo la viwanda Njiro jijini Arusha, inatengeneza magari makubwa ya kubeba watalii maarufu kwa jina la ‘War Bus’. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Satbir Hanspaul, magari hayo yanauzwa Kenya, Afrika Kusini, na nchi za Ulaya.

HAL imesema, imebuni na kutengeneza magari ‘spesho’ ya kubeba takataka yanayofaa kwa mazingira ya Tanzania ikiwemo hali ya hewa, aina ya barabara na mfumo wa maisha wa wananchi hivyo yatadumu kwa muda mrefu.

“Lakini aina mpya ya malori ya kubeba takataka si kwa ajili ya kampuni yetu au kiwanda chetu tu, kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na TBS (Shirika la Viwango Tanzania), wazalishaji wengine wanaweza kuyatengeneza lakini kwa kutumia utambulisho wa ubunifu wa HAL kama kielelezo,” alisema Hanspaul.

Alisema, magari ya kubeba takataka na yale ya watalii ni ubunifu wa Tanzania unaozivutia nchi nyingine zikiwemo za Ulaya, na kwamba magari ya watalii yanakubalika kwenye soko la kimataifa.

Magari hayo yenye nembo za Toyota, Nissan na Land Rover yanatengenezwa kwa kutumia mashine za kisasa zikiwemo robot kama ilivyo kwenye viwanda vya magari katika nchi zilizoendelea.

HAL ilianzishwa mwaka 2007. MAGARI YA KENYA Viwanda vya kutengeneza magari havitakuwa Tanzani na Rwanda tu, kwa kuwa kampuni ya VW tayari ina kiwanda Thika nchini Kenya.

VW ilianza kutengeneza magari Kenya mwaka 2016. Mwaka mmoja baadaye VW ilikuwa imeuza magari 104 nchini humo. Mwaka jana, kampuni ya kutengeneza magari ya Peugeot ya Ufaransa ilianza kutengeneza vyombo hivyo vya usafiri nchini Kenya.

Kampuni ya Toyota ya Japan pia ina kiwanda cha magari nchini humo kilichoanzishwa mwaka 2015. VW wanapanga kuongeza uzalishaji mara mbili katika kiwanda cha Thika sanjari na kutengeneza aina mpya ya gari.

Hivi karibuni, Mkuu wa VW Afrika Kusini na operesheni za kampuni hiyo Afrika, Schaefer alimweleza Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya mjini East London, nchini Afrika Kusini kuwa wapo kwenye mchakato wa kutengeneza aina ya pili ya ga