Reli Isaka-Kigali kuokoa mil. 3.3/- kila kontena

RELI ya kisasa inayotarajiwa kujengwa na kuziunganisha Tanzania na Rwanda kuanzia Isaka mkoani Shinyanga hadi Jiji la Kigali, Rwanda ni ya mapinduzi ya kihistoria kiuchumi.

Mapinduzi hayo yanatokana na ukweli reli hiyo itapunguza sana gharama za usafirishaji mizigo. Kwa Rwanda, inakadiriwa kuwa reli itakapoanza kutumika, itapunguza gharama za usafirishaji kwa wastani wa Dola za Marekani 1,500 (Sh milioni 3.3 za Tanzania) kwa kila kontena, hivyo kuleta unafuu wa bidhaa kwa watumiaji.

“Ni mradi wa kipekee kwa vyovyote unavyoweza kuuzungumzia,” alisema Jean de Dieu Uwihanganye, Waziri wa Nchi Wizara ya Miundombinu (Usafirishaji) wa Rwanda. Mbali ya kauli ya waziri huyo, jamii ya wafanyabiashara Rwanda imeelezea kuguswa na mradi huo wanaouita `Mapinduzi ya Kiuchumi’.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, mradi huo ni wa mapinduzi kwani utarahisisha usafirishaji bidhaa, kupunguza gharama na mkombozi kwa nchi isiyofikika kupitia majini. Deus Kayitakirwa, mmoja wa wakurugenzi Shirikisho la Sekta Binafsi Rwanda (PSF), alisema reli hiyo ya kisasa itaondoa changamoto za wafanyabiashara wa Rwanda.

Kauli ya Waziri Uwihanyange na ile ya wafanyabiashara wa Rwanda, imekuja siku chache baada ya Rais John Magufuli wa Tanzania na Rais Paul Kagame wa Rwanda, kuamua kuziunganisha nchi hizi kwa reli ya kisasa ‘ standard gauge’.

Marais hao walitangaza uamuzi huo Ikulu, Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Rais Kagame nchini, huku wakiwaagiza mawaziri wa pande zote kukutana haraka ili kazi ianze kwa kuwa upembuzi yakinifu na michakato mingine imeshafanyika tangu 2017.

Hatimaye mawaziri hao walikutana mwishoni mwa wiki na kuafikiana kuanza mchakato wa kukusanya fedha, huku jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa reli itakayoanzia Isaka-Kigali ukipangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kwa upande wa Tanzania, reli hiyo itaanzia Isaka, Kahama mkoani Shinyanga ambako itakuwa sehemu ya reli inayoanzia Dar es Salaam na kwenda mikoa mbalimbali ikiwemo ya Kigoma na Mwanza. Reli ya Isaka-Kigali inatarajiwa kuwa ya umbali wa kilometa 521.

Waziri Uwihanganye alisema mazungumzo ya mradi huo, unaotarajiwa kuzigharimu nchi hizo mbili Dola za Marekani bilioni 2.5 (sawa na Sh trilioni sita za Tanzania) yanaendelea vizuri. “Huu ni mradi wenye umuhimu wa kipekee.

Utakapoanza utaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi ndiyo maana tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha mradi unaanza haraka iwezekanavyo,” alisema Uwihanganye. Alisema reli ya Isaka - Kigali ni moja ya miradi mikubwa na ya kipekee, ambayo Rwanda inaelekeza nguvu zake katika Afrika Mashariki.

“Faida ni nyingi mno. Itarahisisha usafiri na usafirishaji, hivyo kushusha gharama za bidhaa kwa kiasi kikubwa. Tutaingia ushindani wa soko la kimataifa. Sitaki kusema mengi, lakini haya ni mapinduzi ya kiuchumi,” alisisitiza.

Kwa sasa, Rwanda inakadiriwa kusafirisha tani 950,000 za mizigo kwa mwaka, kiasi ambacho kitapaa zaidi reli ya kisasa itakapoanza kazi. Pamoja na kiasi hicho kikubwa cha mizigo, Rwanda imedaiwa kuwa na wakati mgumu kiushindani na nchi nyingine kutokana na changamoto ya gharama kubwa za usafirishaji.

Kati ya nchi sita, nyingine zinafikika kirahisi. Mathalani, Kenya ina bahari ya Hindi kama ilivyo Tanzania. Burundi haina bahari lakini hupitisha mizigo yake bandari ya Dar es Salaam, kisha kusafirishwa kwa reli hadi Kigoma inakopakiwa katika meli Ziwa Tanganyika.

Uganda inanufaika pia kwa barabara, lakini pia kwa usafiri wa majini kwa kupitishia mizigo yake Ziwa Victoria, Mwanza ambako mizigo hufikishwa kwa treni inayotoka Dar es Salaam.

Wasafirishaji wa mizigo wa Rwanda wanasema kwa wastani, huwagharimu Dola za Marekani 4,990 (Sh milioni 11 za Tanzania) kusafirisha kontena la urefu wa futi 20 wakati katika nchi nyingine na kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kontena la aina hiyo, gharama yake inakadiriwa kuwa Dola 2,504 (Sh milioni 5.5 za Tanzania).

Hata hivyo, Waziri Uwihanganye alisema kwa sasa gharama ya kusafirisha kontena moja kati ya Kigali na Dar es Salaam ni wastani wa Dola za Marekani 3,912 (Sh milioni 8.6 za Tanzania).

Naye Kayitakirwa, akizungumzia neema ya ujio wa reli hiyo, alisema itapunguza gharama hizo kwa wastani wa Dola 1,500 kwa kila kontena. “Unaona hapo, kiwango cha usafirishaji mizigo mingi kwa mpigo kitaongezeka, lakini gharama zitakuwa chini hivyo kushusha bei ya bidhaa zitakazoletwa Rwanda ni neema,” alisema.

Alipotakiwa kulinganisha umbali kati ya Dar es Salaam-Kigali upande wa Korido ya Kati na ile ya Korido ya Kaskazini, Mombasa- Kampala-Kigali, Kayitakirwa alisema; “Ya Kaskazini ni ndefu, kilometa 1,661 na ina mipaka miwili ya kuvuka tofauti na Korido ya Kati inayolazimu kupita mpaka mmoja wa Rusumo, tena umbali ni kilometa 1,495 tu.”

Kwa mujibu wa Shirika la Taifa la Takwimu la Rwanda, bandari ya Dar es Salaam ndiyo inayotumika kupitisha mizigo mingine ya Rwanda kwa zaidi ya asilimia 80, wakati ile ya Mombasa mizigo ni wastani wa asilimia 20 na 30.

Theodore Murenzi, dereva na mmoja wa wasafirishaji wa mizigo wa Rwanda, alisema malori kati ya 200 na 250 huvuka mpaka wa Rusumo kuingia au kutoka Rwanda na Tanzania kila siku.

“Bandari ya Dar es Salaam ni maarufu, ni muhimu mno kwa wafanyabiashara wa Rwanda kwa sababu ni rahisi na haina vikwazo vingi vya njiani…ukianza safari una uhakika wa kufika bila ya usumbufu,” alisema Murenzi.

Msafirishaji mwingine wa Rwanda, Issa Mugarura, alisema usafiri wa reli utaleta nafuu kubwa ya usafirishaji bidhaa, lakini pia unafuu wa gharama mbali ya kupunguza siku za safari.

Mathalani, reli ya kisasa ya abiria itatumia siku moja au chini ya hapo kati ya Dar es Salaan na Kigali wakati kwa basi, abiria husafiri kwa siku mbili hadi tatu, wakati kwa mizigo treni itasafiri kati ya siku mbili na tatu wakati kwa malori, ni siku nne na tano kutoka Dar es Salaam - Kigali.

Aidha, kwa kutumia treni, mizigo inayoweza kusafirishwa kwa safari moja kati ya nchi hizo ingelazimu kutumia malori hadi 500 kwa barabara na kusababisha uharibifu wa barabara, matumizi makubwa ya mafuta, muda, gharama za usafirishaji kuwa juu na kadhalika.

“Lakini haina maana kwamba tunaipa kisogo reli ya Korido ya Kaskazini. Tunajua Kenya na Uganda zimefikia hatua fulani ya ushirikiano, kwa hiyo nasi tunasubiri kujua nafasi yetu ya kucheza tuweze kufikika kila upande,“ alisema.

Tayari Rwanda imeanza kujenga vituo kadhaa vikubwa vya stesheni za reli nje ya Jiji la Kampala. Stesheni kubwa ya abiria inajengwa Ndera, wilayani Gasabo wakati ile ya mizigo inajengwa Masaka, wilayani Kicukiro.

Waziri wa Miundombinu, James Musoni alithibitisha kuanza mchakato huo, akisema Oktoba mwaka huu Rais Kagame na Rais Magufuli wanatarajiwa kuweka jiwe la msingi la uzinduzi wa ujenzi wa reli ya Isaka - Kigali.

Unafuu wa bidhaa Kayitakirwa alitabiri kuwa, kuanza kwa safari za treni ya Isaka – Kigali, kutaleta unafuu mkubwa wa bidhaa na huduma nchini Rwanda, kwani kwa sasa karibu asilimia 40 ya gharama za uagizaji bidhaa zinaingia moja kwa moja katika usafirishaji na gharama nyingine, jambo linalochangiwa na umbali kati ya Rwanda na bandari za nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Katika nchi zilizoendelea kama China, usafirishaji hugharimu kati ya asilimia 6 na 12. Lakini Kayitakirwa alisema reli ya Isaka –Kigali, itaweza kupunguza hadi asilimia 10 na 15 tu kutoka asilimia 40 ya sasa ya gharama hizo.