Bandari Dar yaweka historia ya mapato

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa, amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, Bandari ya Dar es Salaam inatarajia kupata mapato halisi ya Sh bilioni 450.

Akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu alisema, mpaka robo mwaka kuanzia Julai hadi Septemba kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Bandari ya Dar es Salaam imezalisha Sh bilioni 207.4 huku matumizi yakiwa ni Sh bilioni 67.9 hivyo kufanya pato halisi kuwa Sh bilioni 139.6.

“Inaonesha sasa Bandari ya Dar imejipanga kuhakikisha kwamba hata matumizi yake yamepunguza kwa kiasi kikubwa. Pia mambo hayajaja bure bali yametokana na uboreshaji wa miundombinu unaoendelea.”

Alisema kwa mwaka 2016/17, bandari zote zilitengeneza Sh bilioni 734.9, matumizi yalikuwa bilioni 446 na salio likiwa ni Sh bilioni 288. Alisema katika Bandari ya Dar es Salaam kuna mradi mkubwa wa kujenga gati namba 1-7 kwa kuongeza kina cha maji ambao utawezesha kuingia kwa meli kubwa yenye kontena 19,000 zenye tani 20 hivyo kushindana na bandari zote za jirani Mbarawa alisema, kwa Bandari ya Mtwara kuna mradi wa kujenga gati jipya lenye urefu wa mita 350 utagharimu Sh bilioni 149 na pia kuboresha bandari za Kyela na nyinginezo.

“Pia kuna mradi wa kununua scana nane ambazo zitasaidia kuangalia kinachoendeleza bandarini, gharama za scana hizo ni Sh bilioni 52,” alisema. Aidha Mbarawa alisema serikali iko katika machakato wa kununua rada nne ambazo zitafungwa Dar, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro na hii gharamu Sh bilioni 93.

“Tumekuwa tunapoteza mapato mengi kwenye sehemu ya madini kwasababu watu wanaingia na ndege ndogo mbazo ni ngumu, tunaamini kwa kuweka randa hizo ndege yeyote itakayoingia katika Tanzania tunaweza kuioana na kukusanya mapato yanayostahili.