Majaliwa awapa somo Chadema

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekishauri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kukata rufaa kwenye vyombo vya sheria, endapo kama hakikuridhika na matokeo ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 nchini, ambapo matokeo yake yalitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) karibuni.

Kauli hiyo ilitolewa na Majaliwa bungeni jana, wakati akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema). Minja alihoji kama ni sera ya serikali kukinyang’anya ushindi chama kilichoshinda na badala yake, kukipa ambacho hakikushinda.

Minja alitoa tuhuma kuhusu matokeo ya Kata ya Sofi Jimbo la Malinyi mkoani Morogoro, ambalo alidai Chadema ilipata kura 1,908 dhidi ya kura 1,878 za CCM na matokeo ya Kata ya Siyoi mkoani Singida, ambako alidai Chadema walipata kura 1,358 dhidi ya kura 1,304 za CCM.

Minja ambaye ni mbunge wa Chadema kutoka mkoa wa Morogoro, alidai kuwa katika kata zote hizo mbili, CCM ilitangazwa mshindi. Waziri Mkuu alisema haamini kwamba Tume ya Uchaguzi, inaweza kutangaza matokeo na kukitangaza chama ambacho hakijashinda kwamba kimeshinda.

Lakini, pia alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na serikali za mitaa, wanazo sheria za kusimamia uchaguzi ambao unafanyika, baada ya kukutana na vyama husika na kuweka utaratibu mzuri wa uchaguzi huo.

“Lakini kama chama hakijaridhika, kwa mujibu wa sheria ndani ya siku 60, kinaweza kukata rufaa ili kutafuta haki hiyo kwenye vyombo vya sheria,” alisema. Uchaguzi mdogo wa Madiwani katika maeneo mbalimbali nchini, ulifanyika katika kata 43 nchini Novemba 26, mwaka jana, ambapo CCM ilishinda katika kata 42 na Chadema iliambulia kata moja ya Ibigi wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.