Maofisa utumishi 5 nje uhakiki vyeti

SERIKALI imewasimamisha kazi maofisa utumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza kwa kosa la kutosimamia vema uhakiki wa vyeti vya ufaulu wa elimu ya kidato cha nne, sita na ualimu.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala wa Bora, Dk Laurean Ndumbaro ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Kwimba, Pendo Malabeja kuwasimamisha kazi na kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa utumishi hao. Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Ndumbaro ametoa maelekezo hayo, baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.

Maofisa waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Christina Bunini na wasaidizi wake wanne ambao ni Edward Cornel, Rey Lema, Julius Kiduli na Clavery R.M. Dk Ndumbaro alisema maofisa hao wameitia serikali hasara kwa kuwaacha watumishi wasio na sifa kuendelea kuwepo kwenye orodha ya mishahara ya watumishi wa serikali.

Taarifa hiyo ya Utumishi iliwataja miongoni mwa watumishi walioachwa ni Ligwa Simon aliyestaafu kwa hiari Januari 4, 2010 na Fundi Sanifu Mkuu, Kalala Seleman ambaye amekiri kufanya udanganyifu kwa Katibu Mkuu, Dk Ndumbaro baada ya kukutana naye katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.

Katibu Mkuu alijiridhisha kuwa maofisa utumishi hao kutozingatia maelekezo ya kuwaondoa watumishi ambao taarifa zao walizojaza wakati wanaajiriwa zinaonesha kuwa wamehitimu na kufaulu kidato cha nne, lakini wakati wa uhakiki, watumishi hao hawakutakiwa kuwasilisha vyeti husika kwa kigezo kuwa wana elimu ya darasa la saba.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa msingi huo na kwa kuzingatia kuwa maofisa utumishi hawakuwataka watumishi hao kuwasilisha vyeti vya elimu walizojaza wakati wanaajiriwa katika fomu ya taarifa binafsi, wamekiuka na kupuuza agizo la Rais John Magufuli la kuwataka waajiri wote nchini kufanya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma na kuwaondoa katika orodha ya malipo ya mshahara ya watumishi wa serikali (Payroll).

Dk Ndumbaro alimtaka Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Kamishna wa Polisi, Clodwing Mtweve kupeleka maofisa utumishi wengine katika Halmashauri ya Kwimba ili kutoathiri utendaji kazi. Pia aliwataka waajiri wote nchini kuhakikisha kazi ya uhakiki wa vyeti vya watumishi inafanyika kwa umakini. Aidha, Dk Ndumbaro aliainisha kuwa, suala hilo litawasilishwa kwa mamlaka ya uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Pendo Malabeja kuona hatua stahiki za kuchukuliwa dhidi yake.