Wadau kukutana kujadili dawa bandia barani Afrika

WADAU wa afya barani Afrika wanakutana kesho jijini Dar es Salaam kuweka mikakati ya kudhibiti utengenezaji na usambazaji wa dawa bandia barani Afrika.

Sehemu ya taarifa ya pamoja iliyotolewa jana na waandaaji wa kongamano la siku nne la Jukwaa Jipya la Ubora wa Dawa Barani Afrika (African Medicines Quality Forum) inasema: “Tunataka kuhakikisha kuwa Waafrika wanatumia dawa salama zenye ubora.

Waandaaji hao ni The United States Pharmacopeia convention (USP), New Partnership for African Development (NEPAD) pamoja na Mamlaka ya Dawa na Chakula Nchini (TFDA). Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anatarajiwa kufungua kongamano linalolenga kuweka mikakati itakayotatua changamoto zitokanazo na matumizi ya dawa zenye ubora hafifu barani Afrika.

Kuanza kwa Jukwaa la AMQF kunakuja wakati kukiwa na ongezeko la matumizi ya dawa bandia na zisizo na kiwango cha ubora na zilizokwisha muda wa matumizi katika sehemu mbalimbali barani Afrika, ikiwemo Tanzania. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) asilimia 42 ya taarifa zinahusu dawa bandia na dawa zilizokwisha muda wake, huripotiwa katika nchi za Afrika.