Kiswahili chashika kasi ughaibuni

KISWAHILI ndiyo lugha ya Kiafrika pekee yenye wanafunzi wengi katika vyuo mbalimbali vinavyofundisha lugha zingine za Kiafrika duniani.

Aidha imeelezwa pia kwamba Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika inayofundishwa katika nchi nyingi za Afrika ambazo hazina wazungumzaji wazawa wa lugha hiyo. Hayo yameelezwa na Dk Rajabu Chipila wa Chuo Kikuu chaDar es Salaam ambaye amebahatika kufundisha lugha hiyo katika vyuo mbalimbali duniani alipofanya mahojiano na gazeti hili hivi karibuni.

Dk Chipila alisema Lugha zingine za Kiafrika zinazofundishwa katika vyuo vingine vikuu duniani ni pamoja na Kihausa na Kiibo (Nigeria), Kiamhariki (Ethiopia), Kisomali (Somalia), Kikuyu (Kenya), Kizulu (Afrika Kusini), Kilingala (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), na Kinyarwanda (Rwanda) “Utandawazi unaulazimisha ulimwengu kufahamu lugha nyingi kadri iwezekanvyo ili kufanikisha malengo mbalimbali kama vile biashara, elimu, utafiti, utamaduni, siasa, ulinzi, na diplomasia,” alisema.

Mhadhiri huyo ambaye amepata kufundisha Kiswahili katika nchi za Korea Kusini, Afrika Kusini, na Ufaransa, alisema kimsingi, Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika yenye wazungumzaji wengi waliosambaa katika nchi tofautitofauti. Lugha nyingine yenye idadi kubwa ya wazungumzaji ni Kihausa cha Nigeria. “Tatizo la Kihausa, ni lugha inayonasibishwa na kabila moja, Wahausa. Kiswahili kinazizidi lugha nyingi za Afrika kwa kigezo hiki cha kuwa ni lugha isiyonasibishwa na kabila lolote,” alisema. Mahojiano rasmi na msomi huyo yamechapishwa kwa kina katika Ukurasa wa 15 wa gazeti hili.