Wanaopita Mikumi huenda wakatozwa kodi

SERIKALI inafikiria namna bora ya kubadilisha uelekeo wa eneo la kilometa 50 za barabara ya lami inayopita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi au kutoza kodi ya utalii kwa watu wanaotumia barabara hiyo.

Lengo la hatua hiyo ni kukabiliana na changamoto mbalimbali, zinazosabishwa na barabara hiyo kwenye uhifadhi.

Hayo yalisemwa jana mkoani Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kufuatia ombi la uongozi wa hifadhi hiyo la kuiomba Serikali kuchepusha barabara hiyo kutokana na athari mbalimbali za kimazingira, zinazosabishwa na barabara hiyo hususani vifo vya mara kwa mara vya wanyamapori na ukosefu wa mapato ya serikali.

Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo mbele ya Waziri Kigwangalla, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald Mono alisema licha ya barabara hiyo kuwa na fursa nyingi za kimaendeleo, imekuwa na changamoto nyingi kwenye uendeshaji wa shughuli za uhifadhi.

Alisema wastani wa mnyamapori mmoja hugongwa na gari kila siku katika barabara hiyo, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2014 idadi ya wanyamapori waliogongwa walikuwa 351, mwaka 2015 walikuwa 361 na mwaka 2016 walikuwa 218.

Alisema changamoto nyingine ni uchafuzi wa mazingira, ambapo wastani wa taka ngumu zisizopungua kilo 138.3 huzalishwa kila siku na watumiaji wa barabara hiyo.

Mbali na changamoto hizo alisema nyingine ni ukosefu wa mapato ya serikali kufuatia kukosekana kwa mageti ya kulipia tozo za utalii kwa watumiaji wa barabara hiyo, ambao hufaidi utalii wa bure na kuikosesha serikali mapato.

Alisema changamoto nyingine ni ujangili, ambao huchochewa na uwepo wa barabara hiyo, ambayo hutoa fursa kwa majangili kuingia katika hifadhi hiyo kiurahisi kwa njia mbalimbali ikiwemo magari na pikipiki.

"Hifadhi inaiomba Serikali kuchepusha barabara hii ili kupunguza changamoto hizi zinazotokana na uwepo wa barabara husika na kuongeza mapato ya hifadhi kwa kuzuia utalii wa bure unaofanywa na watumiaji wa barabara wa ndani na nje," alisema Kaimu Mhifadhi Mkuu huyo wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Waziri Kigwangalla alisema changamoto kubwa aliyoiona katika hifadhi hiyo ni namna ya watalii kufika na kufanya shughuli za utalii katika hifadhi hiyo.

Alisema licha ya uwepo wa barabara ya lami inayokatiza hifadhini hapo, barabara hiyo si rafiki kwenye uhifadhi.

"Kuna hiyo barabara ambayo inaleta watalii hapa, ni barabara ambayo iko bize sana, ni barabara ya kitaifa na kwa vyovyote vile hii si barabara mahsusi kwa ajili ya shughuli za utalii.

"Sisi (serikali) tunatafakari namna ya aidha kuiondoa hiyo barabara au namna ya kuwachaji watu wanaokatiza hizi kilometa 50 ambazo zipo ndani ya Hifadhi ya Mikumi," alisema Dk Kigwangalla.